
Mhariri Msanifu wa Gazeti la
Mtanzania, Khamis Mkotya, akiangalia kisima kilichochimbwa katika Kijiji
cha Chandama wilayani Chemba, chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo
la Japan (JICA), kikiwa kimepigwa kufuli. Katikati ni mkazi wa kijiji
hicho, Igwana Maulid na Yusuph Kijuu. Na Mpigapicha Wetu
……….
Na Mwandishi Wetu, Chemba
WANANCHI wa Kijiji cha Chandama,
Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, wameshindwa kufanya shughuli za
maendeleo, kutokana na kukabiliwa na tatizo la maji kwa miaka mingi.
Wananchi hao walisema, wanashangaa
kuona wanapata shida ya maji, wakati kuna visima viwili vilivyochimbwa
kijijini hapo na vyenye maji mengi, lakini hawafaidiki navyo kutokana na
ukosefu wa miundombinu.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi kwa nyakati tofauti na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, walipokuwa wakizungumza na MTANZANIA.
Kutokana na shida hiyo, wananchi
hao wamemwomba Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge,
afike kijijini hapo ili aweze kutatua kero hiyo iliyodumu kwa muda
mrefu.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho,
Iddy Ijui, alisema kijiji hicho kinakabiliwa na shida kubwa ya maji,
ambapo hivi sasa wanalazimika kununua pipa moja la maji kwa Sh 5,000.
“Kitendo cha kukosa maji kinatufanya tushindwe kufanya shughuli za maendeleo, kwani tunapoteza muda mwingi kutafuta maji.
“Hapa kijijini kuna visima viwili
na vyote vina maji mengi, lakini vimefunikwa na magunia na kingine
kimepigwa kufuli tangu 2011, sasa hatuelewi lengo lao lilikuwa ni
kutuachia mashimo au kutoondolea kero ya maji,” alihoji.
Naye Igwana Maulidi, alisema
katika kujitafutia huduma hiyo wananchi wa kijiji hicho wamechimba
visima virefu vya kienyeji vinavyotumia kamba, kiasi cha kuhatarisha
usalama wao.
“Visima viwili vimechimbwa lakini
havitumiki, hatuwezi kupata maji kwa sababu havijafungwa mashine. Kibaya
zaidi hakuna kiongozi anayezungumzia hatima ya hivi visima na jitihada
za kumaliza hii kero, ndiyo maana tunaomba waziri wa maji aje hapa
kijijini,” alisema.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho,
Mustafa Kidunka maarufu kwa jina la Munguji, alisema wananchi wa kijiji
hicho ni kama yatima, kwani hakuna kiongozi anayehangaika kutatua kero
zao.
“Watu wanashida ya maji hakuna
anayejali, kilichimbwa kisima hapa na wajapani, kimepigwa kufuli hadi
leo hakijafunguliwa. Mwaka jana tena halmashauri ilichimba kisima
kingine na chenyewe kimefunikwa tu, kama ni hasara ya viongozi
tumeipata,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Kijiji hicho, Said Mwaliko (Chadema), maarufu kwa jina la Machapati,
alikiri kuwapo kwa kero hiyo na kusema uongozi wa juu ndiyo kikwazo cha
kumaliza kero hiyo.


No comments:
Post a Comment