KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

November 1, 2016

SERIKALI YATENGA MABILIONI KUJENGA MAHAKAMA

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEggxXKWsM77VzulbKM5wGgaxDKs4WUSLhYfHuaElS2JCl5tD5Y0aA-M91BjX93UZtWqtkSXPnMcQ8hFfjkcQHOZZTcykkyfT9RVrWyiJTiaXNoDoy8-E6NGQyUujaupN9NDYtxde6j9OaA/s1600/unnamed.jpg
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.

Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 48.3 kwa ajili ya kujenga Mahakama 40 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ili kuongeza ufanisi na kuharakisha hukumu za kesi katika ngazi mbalimbali  chini.

Kutokana na fedha  itakayotumika kujenga mahakama, shilingi bilioni 36 zinatokana na Bajeti ya mwaka huu wa fedha wakati shilingi bilioni 12.3 zilitolewa na Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.

Hayo yamebainishwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dkt. Harisson Mwakyembe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Iramba  Mashariki Mhe. Allan Kiula  aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itatoa  fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya na uteuzi wa Mahakimu  katika ngazi hiyo.

Waziri Mwakyembe amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Mahakama zinakuwepo kila wilaya ili kuwaondolea  usumbufu wananchi, kurahisisha usikilizwaji wa kesi pamoja na kupunguza gharama kwa wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine kufuata Mahakama
zilipo.“Kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Sheria na Kanuni inaeleza kuwa kila Mahakama ina mipaka yake hivyo hatuwezi kubadilisha mahakama ya mwanzo kutumika kama ya wilaya” amesema Dkt. Mwakyembe.

Ameongeza kuwa mpaka sasa bado kuna wilaya zinapata huduma ya Mahakama kupitia wilaya nyingine ambapo amewahakikishia Wabunge na wananchi kuwa Serikali itajenga mahakama 40 kwa mwaka huu wa fedha.

Akifafanua mgawanyiko wa Mahakama 40 zinazotarajiwa kujengwa nchini, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Serikali itajenga Mahakama Kuu nne, Mahakama za mikoa sita, Mahakama za Wilaya 14 na Mahakama za Mwanzo 16 katika wilaya mbalimbali nchini.

Aidha, Mhe. Mwakyembe ametaja baadhi ya vigezo vinavyotumika kuanzisha Mahakama katika eneo lolote kuwa pamoja na  uwepo wa hati ya kisheria ya kuwepo kwa wilaya, mkoa, kata na kijiji,  umbali wa upatikanaji wa huduma za Mahakama, idadi ya wakazi wa eneo husika pamoja na uwepo wa huduma zingine za kipolisi na magereza.

Ameongeza kuwa kutokana na changamoto hizo za kukosekana kwa mahakama katika maeneo ambayo yamekidhi vigezo ndiyo yaliyopelekea Serikali kujipanga  kujenga Mahakama hizo  ambapo ametoa rai kwa wananchi kuwa na subira wakati wakikusubiri kujengwa kwa Mahakama hizo.

No comments:

Post a Comment