o Ni kupitia mradi wa kutokomeza vifo vya akina mama wajawazito na
watoto wachanga
o Na kurahisishwa na Huduma ya M-Pesa ya Vodacom
Wakina mama wajawazito na watoto wa wilayani Sengerema wamefarijika
baada ya kujionea manufaa ya mradi wa kutokomeza vifo vya akina mama hao na
watoto wachanga ukiendelea vizuri na kuleta mabadiliko makubwa katika jamii yao
inayowazunguka,Mradi huo ambao ulizinduliwa mwaka jana wilayani humo
chini ya ufadhili wa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana
na mashirika ya kimataifa ya USAID, Path Finder na Touch Foundation
unazidi kuleta mafanikio makubwa katika wilya hiyo.
Moja ya mafanikio makubwa ambayo yamepatikana kupitia mradi
huu ni kuokoa maisha ya wanawake wajawazito na watoto wachanga wapatao 580
pia umewezesha mafunzo kwa wahudumu wa Afya wa ngazi ya Jamii wanaopita
kila kaya kutoa elimu, ili kubadili mitazamo hasi ya baadhi ya akina mama
kutofika kwenye vituo vya afya kupatiwa huduma za uzazi na akina mama zaidi ya 6,000
wamepatiwa elimu hii.
Wafadhili wa mradi huu wamekuwa wakigharamia mafunzo kwa
wahudumu wa afya na usafiri wa akina mama wajawazito wanaokaribia kujifungua
kuwawahisha kwenye vituo vya afya kupata matibabu ya haraka pindi
panapohitajika msaada ambapo wameingia mkataba maalumu na madereva wa teksi
katika kufanikisha mradi huu ambao hutoa huduma hii kwa haraka na kulipwa
kupitia huduma ya M-Pesa.
Mkazi wa Sengerema Mwanza Kwangu Jackson, ambaye ni mmoja wa
wanawake walionufaika akiongea kwa niaba ya wanufaika wa mradi
aliupongeza mradi huu na kusema ni mkombozi kwa akina mama wengi na
ulimsaidia alipokuwa mjamzito na kwenye hali ya uchungu. Alipopiga simu aliweza
kusaidiwa mara moja na amejifungua salama kabisa na anatoa wito kwa wanawake
wengine wengi zaidi kujitokeza kunufaika na huduma hii.
“Kipindi changu cha ujauzito kiligubikwa na changamoto
mbalimbali ,ulipofikisha miezi 8 nilianza kusikia maumivu makali kwenye kiuno
na nilitembea umbali wa kilometa 2 hadi kituo cha afya ambapo mhudumu aligundua
kuwa nilitakiwa kujifungua kwa njia ya operesheni na kulazimika kunihamishia
katika hospitali ya wilaya iliyopo umbali wa Kilometa 55 ambapo nilisafirishwa
na teksi iliyopo chini ya mradi huu ambayo ilitumia muda wa masaa 2
kufika hospitalini hapo ambapo niliweza kujifungua salama.Bila huduma hii
ningepoteza maisha yangu na mtoto”.Alisema.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa mradi huu,Naibu Waziri wa
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Dk.Hamis Kingwangalla,aliwapongeza
wadau wote walioufanikisha na kuwa unaenda sambamba na malengo ya
serikali ya kutokomeza matukio ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto
wachanga nchini.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom
Tanzania,Rosalynn Mworia,alisema mfuko wa kusaidia jamii wa kampuni hiyo pamoja
na kampuni kwa ujumla inajivunia kuona mafanikio makubwa yanapatikana
katika kipindi kifupi cha mradi huu wenye lengo la kuunga mkono
jitihada za serikali za kuboresha sekta ya afya nchini na adhma ya kutokomeza
vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga nchini.
“Mradi huu ambao unajulikana kama”MOYO” awamu ya pili umelenga
kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha sekta ya afya nchini na adhma ya
kutokomeza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga nchini pia
umelenga kurejesha fadhila kwa wateja wetu, tutagharamia usafiri wa akina mama
wajawazito kupitia huduma ya M-Pesa kama ambavyo ilikuwa kwenye awamu ya kwanza
ya mradi ili waweze kufika kwenye vituo vya afya kupata matibabu haraka“,Alisema.
No comments:
Post a Comment