![]() |
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa
mahojiano maalum na televisheni ya Taifa (TBC) katika maadhimisho ya
Siku ya Wanawake Duniani, nyumbani kwake Makao Makuu ya Nchi Dodoma
(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amelaani na kukemea vikali
vitendo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinavyoendelea katika jamii
na amewataka wananchi kote nchini kushirikiana katika kukabiliana na
vitendo hivyo nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo tarehe
8-March-2017 wakati akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la
Utangazaji wa Tanzania (TBC) mjini Dodoma kuhusu maadhimisho ya siku ya
wanawake Duniani.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amesema vitendo hivyo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji
vinamchukiza sana hivyo ametoa wito maalum kwa wananchi na wadau wote
bila kujadili dini, kabila wala rangi kupambana ipasavyo na vitendo
hivyo ambavyo vinarudisha nyuma jitihada za kumkwamua mwanamke kiuchumi.
Kuhusu maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema
anafurahishwa na hatua na jitihada zinazochukuliwa na wanawake kote
nchini katika kujikwamua kiuchumi kwa kuimarisha shughuli zao za
ujasiriamali katika kuelekea katika uchumi wa viwanda.
Amesema jukumu kubwa la serikali
ya awamu ya Tano ni kuhakikisha wanawake wanaboreshewa ipasavyo
mazingira ya kufanyia kazi hasa shughuli za ujasiriamali ili waweze
kufikia malengo waliyojiwekea.
“Inapofika katika shida zetu
wanawake ni lazima tuwe na kitu Kimoja na sauti Moja katika kulinda na
kutetea haki zetu bila kujali itikadi za kisiasa”Amesisitiza Makamu wa Rais.
Katika uundaji wa majukwaa ya
kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amesema kazi hiyo inaendelea vizuri na kutaka mikoa na wilaya
ambazo bado haijaunda majukwaa hayo kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.
Ameeleza kuwa lengo la uundaji wa
majukwaa hayo katika ngazi ya wilaya na mikoa nchini ni kuwakutanisha
wanawake pamoja katika kujadili na kutafutia ufumbuzi changamoto
zinazowakabili ikiwemo tatizo la masoko za bidhaa wanazozizalisha.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amesisitiza kuwa majukwaa hayo ambayo yameanza kuundwa katika
mikoa mbalimbali nchini yatakuwa sio ya kisiasa.
Katika Mahojiano hayo na
mtangazaji Shaban Kissu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mjini
DODOMA, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu ametumia sehemu ya mahojiano
hayo kwa kuwatakia heri na mafanikio wanawake wote nchini katika
kuadhimisha Siku ya wanawake Duniani.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake Duniani ni “Tanzania ya Viwanda,Wanawake ni msingi wa mabadiliko ya Kiuchumi”.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dodoma.
8-Mar-2017
|
March 8, 2017
MAKAMU WA RAIS AKEMEA VITENDO VYA UKEKETAJI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment