Kwa
mara ya kwanza, Alicia Magabe ambaye ni mke wa Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amezungumzia tukio la mumewe
kushambuliwa kwa risasi na kudokeza kwamba haliwezi kuwa limetokana na
sababu nyingine isipokuwa kazi ambazo amekuwa akizifanya.
Pia amezungumzia kuhusu afya yake na kueleza kuwa bado siyo nzuri na kuwaomba Watanzania waendelee kumuombea.
Mbali
ya Alicia ambaye pia ni mwanasheria, dereva wa Lissu naye amezungumza
akisema ameathiriwa kwa kiasi kikubwa na tukio hilo huku akiahidi
kuripoti polisi mara baada ya kurejea nchini.
Lissu
ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), amelazwa
katika Hospitali ya Nairobi tangu alipopelekwa huko baada ya kupigwa
risasi akiwa ndani ya gari nje ya nyumba yake mjini Dodoma mchana wa
Septemba 7 akitokea bungeni.
“Watanzania
wote wanajua Lissu maisha yake yote amekuwa ni mtetezi wa wanyonge na
tukio hili amelipata kutokana na kazi zake hizo hivyo nawaomba tumuombee
tu,” alisema.
“Ninachoweza
kusema hali ya mheshimiwa Lissu sio nzuri ingawa ni tofauti na
tulivyomleta hapa, hivyo naomba Watanzania kuendelea kumuombea.”
Aliwashukuru
Watanzania kwa michango, na maombi yao kwa Lissu akisema hiyo
inaonyesha ni jinsi gani wanathamini mchango wake kwa jamii.
Alipoulizwa
kuhusu kauli ya Serikali kwamba ipo tayari kugharimia matibabu ya Lissu
popote ikiwa itaombwa na familia hiyo, Alicia ambaye pia ni wakili
alisema kwa sasa hana maoni.
“Katika
hili no comment (sina maoni) ndio tumesikia jana amezungumza na kwa
kuwa jambo hili siyo la uamuzi wa mtu mmoja, mimi sina cha kusema,”
alisema.
Hata
hivyo, alisema anashukuru kazi kubwa ambayo inafanywa na madaktari wa
Hospitali ya Nairobi na kusema wanaridhishwa na matibabu ambayo
anapatiwa kwa sasa.
Kauli ya Dereva wa Lissu
Mbali
ya Alicia, dereva wa Lissu ambaye ndiye mtu pekee waliyekuwa wote siku
ya tukio hilo, Simon Bakari naye alizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu
tukio hilo na kudokeza kwamba limevuruga na hana kumbukumbu sahihi.
Dereva
huyo ambaye naye anaendelea kupatiwa matibabu ya kisaikolojia katika
hospitali hiyo ya Nairobi alisisitiza, “Kwa sasa siwezi kuzungumza
vizuri tukio hili kwani nadhani sina kumbukumbu vizuri.”
Alipoulizwa kuhusu wito wa polisi wa kwenda kutoa maelezo, alisema atafanya hivyo pindi atakaporejea nchini baada ya matibabu.
“Nilisikia polisi wamenitaka nikatoe maelezo lakini sijisikii vizuri na bado napata matibabu. Nitakwenda,” alisema.
No comments:
Post a Comment