Serikali imekitaka Chuo Cha Utumishi wa Umma
Tanzani (TPSC) kufanya tafiti, kutoa mafunzo na kutoa ushauri unaolenga
kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kwa sasa ikiwamo
umasikini.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika mahafali ya
27 ya TPSC kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora) Angellah Kairuki, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi alisema kuwa mafunzo
yanayotolewa na chuo hicho pia yalenge katika kukabiliana na Rushwa, mmomonyoko
wa maadili na kufanya kazi kwa mazoea katika sekta ya umma.
“Ni matumaini yangu kuwa aina ya mafunzo na shauri
za kitaalam zinazotolewa na zinazoendelea kutolewa na chuo hiki zitakwenda
sambamba na maboresho katika sekta ya umma na pia kuwawezesha watumishi wa
serikali na na wale watakaoingia serikalini siku za usoni kukabiliana na
mabadiliko yanayoendelea hapa nchini na Duniani kote,” alisema
Alisema kuwa katika kuelekea Tanzania ya Viwanda
serikali inasisitiza mafunzo na tafiti zinazofanywa na chuo hicho kujikita
katika kuandaa watu mahiri , wenye weledi na ujuzi utakaotumika kuisaidia
kuendana na kasi ya ukuaji wa viwanda na hivyo kutimiza ndoto za Rais Dkt.John
Pombe Magufuli za kujenga Tanzania ya Viwanda.
Alisema kuwa serikali inaunga mkono jitihada mbalimbali
zinazofanywa na taaisi hiyo zenye lengo la kuboresha huduma mbalimbali
zitolewazo na chuo baadhi ya maboresho hayo yakiwa ni kuanzishwa ka kozi za
shahada katika fani za Uhazili na Menejimenti ya Kumbukumbu,Ukamilishaji wa
mchakato wa ujenzi wa jengo la Maktaba katika Tawi la Tabora sanjari uandaaji
wa mpango wa ujenzi (Master Plan) Tawi la Singida.
Awali katika Mahafali hayo Mtendaji Mkuu wa TPSC
Dkt.Henry Mambo alisema kuwa wahitimu
6332 walihitimu mkatika mahafali hayo wakitoka katika matawi sita ya chuo hicho
yaliyoko katika mikoa ya Singida, Dar es Salaam, Mtwara, Tanga,Mbeya na Tabora.
Dkt. Mambo alizitaja aina za vyeti na idadi ya wahitimu
kwenye mabano kuwa ni Astashahada ya Awali (2,368),Astashahada (1,781) na
Stashahada (2183).
Alisema katika kuelekea Uchumi wa kati, ifikapo
mwaka 2025 chuo kimeendela kuboresha huduma zake mbalimbali ikiwamo usimikazi
wa utoaji elimu bora yenye viwango vya
kukidhi hali ya soko la ajira na kiushindani.
“Pia tunaendeleza watumishi wetu ili wafikie
viwango vinavyohitajika,” alisema.
Mkuu huyo wa Chuo alisema kuwa TPSC imeendelea
kufanya vizuri katika eneo la tafiti na machapisho na shauri za kitaalam ili
kubaini changamoto zilizopo katika utumishi wa umma na kutoa majawabu ya
changamoto hizo kupitia tafiti.
No comments:
Post a Comment