Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, George Mkuchika amesema ana mpango wa kupeleka bungeni maombi ya
kuongezwa muda wa kustaafu maprofesa.
Amesema
umri wa kustaafu kwa sheria unawafanya wasomi hao washindwe kutumika
vizuri kulijenga Taifa, hivyo ataomba wastaafu wakiwa na umri wa miaka
65 badala ya 55.
Mkuchika
amesema hayo leo Jumatatu Oktoba 16, alipotembelea ofisi za
Sekretarieti ya Ajira na kukutana na watendaji wa taasisi hiyo.
Amesema baadhi ya kada ambazo zinafanyiwa kazi na maprofesa zinatakiwa kuangaliwa kwa jicho la tofauti.
Waziri amesema wengi wanapata uprofesa wakiwa na miaka 55 na hufanya kazi kwa miaka michache na kutakiwa kustaafu.
"Tutapeleka
bungeni maombi kuwe na mabadiliko kidogo katika baadhi ya maeneo, hawa
maprofesa wengi wanaofikia hatua hiyo wanakuwa na miaka kuanzia 50 na
kuendelea halafu anafanya kazi kidogo anatakiwa kustaafu," amesema.
Amesema
haitakuwa na maana kama wasomi hao wanatumia rasilimali za Taifa
kufikia hatua hiyo halafu baada ya kuhitimu wanafanya kazi kwa muda
mfupi na kutakiwa kustaafu.
Mkuchika amesema pia atawasilisha maeneo mengine ambayo yana upungufu unaotokana na sheria.
Amesema
hayo akijibu changamoto iliyotolewa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira,
Xavier Daudi ambaye ameeleza kuwa sheria inatoa mwanya kwa taasisi
nyingine za umma kuajiri bila kupitia sekretarieti hiyo.
"Kuna
mgongano wa kisheria kati ya sheria iliyoanzisha Sekretarieti ya Ajira
na baadhi ya taasisi za umma ambazo nazo zina mamlaka ya kuajiri
watumishi kwenye taasisi zao," amesema Daudi.
Akijibu
hilo, Mkuchika amesema, "Naahidi katika kipindi changu cha uwaziri
nitafanyia kazi changamoto hiyo na ikiwezekana maeneo yote yawekwe sawa
kisheria."
Mkuchika amewaasa watendaji wa taasisi hiyo kujiweka mbali na vitendo vya rushwa.
"Fanyeni
kazi bila upendeleo, jiwekeni mbali na rushwa natambua hakuna sehemu
yenye changamoto ya rushwa kama Sekretarieti ya Ajira. Usiombe faili
lako lije kwangu eti mfanyakazi wa sekretarieti ya ajira ana kesi ya
rushwa," amesema.
Waziri
amesema, "Nitasimamia utendaji wa watumishi wa umma, tufanye kazi
kulingana na malipo tunayolipwa na kodi za Watanzania. Nafahamu wapo
watumishi wa umma ambao wanalipwa mshahara ilhali hawafanyi kazi
inavyostahili."
Kuhusu
watumishi wa umma walioshiriki na kushinda katika uchaguzi ndani ya
Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema watawashughulikia kulingana na
mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi.
Amesema
wakati nchi inaingia kwenye mfumo wa vyama vingi, Katibu Mkuu Kiongozi
alitoa mwongozo ambao ulielekeza kuwa kuna baadhi ya watumishi wa umma
kulingana na nafasi zao wapo wanaoruhusiwa na wasioruhusiwa kushiriki
kwenye siasa.
No comments:
Post a Comment