KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

February 25, 2018

RAIS MAGUFULI AZUNGUMZIA UPANUZI WA UWANJA WA NDEGE WA MWANZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amerejea nchini  tarehe 24 Februari, 2018 akitokea nchini Uganda ambako amehudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliomalizika jana Mjini Kampala.

Katika uwanja wa ndege wa Mwanza Mhe. Rais Magufuli amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. John Mongella aliyeongozana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Antony Dialo.

Akiwa uwanjani hapo Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Mwanza ambao wamemuomba asaidie kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili uwanja huo zikiwemo mahitaji ya jengo la abiria kutokana na jengo lililopo kuwa dogo, mahitaji ya ujenzi wa uzio wa kuzunguka uwanja na ndege zinazobeba minofu ya samaki kutotumia uwanja wa Mwanza na badala yake kutumia viwanja vya nchi jirani kutokana na ongezeko la tozo ya kodi kwa ndege hizo.

Katika majibu yake Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi mahitaji ya kujengwa kwa jengo la abiria pamoja na ujenzi wa uzio ili uwanja wa Mwanza uwe na hadhi ya kimataifa na hivyo kuiwezesha nchi kupata mapato zaidi.

Kuhusu changamoto ya ndege za kubeba minofu ya samaki kutotumia uwanja wa Mwanza Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itafanyia kazi jambo hilo na kulitafutia ufumbuzi haraka ili ndege hizo zitumie uwanja huo na kuiingizia nchi mapato.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema anasubiri ripoti ya Wizara ya Ardhi kuhusu wananchi waliovamia uwanja wa ndege wa Mwanza lakini amebainisha kuwa Serikali haiwezi kukimbilia kuondoa kaya zaidi ya 1,900 zinazodaiwa kuvamia eneo hilo na badala yake itaangalia njia bora ya kufanya.

Hata hivyo ametaka wananchi waliopo katika eneo hilo wasiendeleze makazi yao wakati uamuzi wa Serikali unasubiriwa.

“Bahati nzuri Naibu Waziri wa Ardhi upo hapa, kafanyieni kazi changamoto hii na mnipe ripoti” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Baada ya kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza Mhe. Rais Magufuli ameelekea nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mwanza
24 Februari, 2018

No comments:

Post a Comment