Ili
kuhakikisha huduma zote zinatolewa kidigitali, Wakala wa Usajili wa
Biashara na Leseni (Brela) umetoa miezi sita kwa wamiliki wa kampuni
kuhakiki taarifa zao kwenye mfumo mpya kwa njia ya mtandao, vinginevyo
hawatapata huduma wanazostahili.
Agizo
hilo linazihusu kampuni 200,000 zilizosajiliwa kabla ya Februari mosi
mwaka huu baada ya mfumo huo kuanza kutumika Januari 4.
Ofisa
mtendaji mkuu wa Brela, Frank Kanyusi alisema mpaka sasa ni kampuni 200
pekee zimesajiliwa kwenye mfumo huo na kufafanua kuwa, hakuna kampuni
itaweza kufanya lolote kwani mifumo yote ya Serikali inaangalia ripoti
ya Brela kabla ya kumhudumia mteja.
“Kama
hujahakiki taarifa na kuingia kwenye mfumo wa mtandao, hakuna chochote
unachoweza kufanya kwa kuwa hata mamlaka nyingine kama (Mamlaka ya
Mapato Tanzania) TRA lazima zije kwetu kujiridhisha kuhusu kampuni
fulani. Hivyo, iwapo haijasajiliwa haitapata huduma,” alisema.
Kwenye
mfumo huo, mmiliki wa kampuni anaweza kufanya mabadiliko yoyote kwa
njia ya mtandao, hivyo kupunguza gharama ya kusafiri kutoka mikoani
mpaka Dar es Salaam zilipo ofisi za wakala huo.
“Sasa
hivi chochote kinafanyika mtandaoni, tukijiridhisha tunaingiza kwenye
nyaraka zetu kama hatujaridhika tunawasiliana na mhusika,” alisema
Kanyusi.
Alisema
kinachotakiwa kampuni kujisajili kwenye mfumo huo ni namba ya
ulipajikodi, namba ya mlipakodi ya kila mkurugenzi, vitambulisho vya
uraia vya wakurugenzi na wenye hisa ndani ya kampuni.
Tangu
mfumo huo uanze kufanya kazi, Kanyusi alisema umerahisisha utoaji
huduma. “Tumeshaanza kupata mrejesho kutoka kwa mawakala wa alama za
biashara, wanasema umewaondolea usumbufu na umewarahisishia utendaji wao
tofauti na ilivyokuwa awali wakati kazi zilipokuwa zikifanyika kwenye
karatasi,” alisema.
Muda
wowote kuanzia sasa, Brela inatarajia kuzindua utoaji leseni daraja A
na B kwa njia ya mtandao, huku ikiwa imejiwekea malengo ya kusajili
zaidi ya kampuni 50 kwa siku kupitia mfumo huo.
Kanyusi
alisema Brela ndiyo mlango wa kurasimisha biashara hivyo inaweka
mazingira rahisi ya kuanzisha biashara na kuvutia wawekezaji.
“Tunafahamu
zitakuwapo changamoto za hapa na pale kwenye mfumo huu mpya ila
ninaamini tutafika, wenye kampuni wazivumilie watakazokumbana nazo ila
wasajili kampuni zao,” alisema.
Mfumo
huo unaotumiwa na Brela unaziunganisha mtandaoni taasisi muhimu za
Serikali zinazohusika na usimamizi wa biashara, ili kuokoa muda kwa
wahusika kuzifuata kwenye ofisi zilizopo maeneo tofauti.
Kanyusi
alisema faida nyingine za mfumo huo ni kupunguza gharama na muda wa
kusajili na kuanzisha biashara nchini. Kabla ya kuanza kuutumia mfumo
huo, Brela ilienda kujifunza kwenye mataifa mbalimbali kuhusu ufanisi
wake ikiwamo Vietnam unakotumika kwa miaka mingi.



No comments:
Post a Comment