Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 24 na 25, 2018 itaanza kusikiliza
ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili
Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido
Mhando.
Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.
Mwendesha
Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Leonard Swai leo Machi 28, ameieleza kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma
Shaidi kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa ushahidi wa
mashahidi wa upande wa mashtaka.
Ameieleza kuwa kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Victoria Nongwa ila kwa sasa imepangwa kusikilizwa mbele yake.
Baada
ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Shaidi ameipanga kuisikiliza kesi
hiyo Aprili 24 na 25, 2018 ambapo upande wa mashtaka umedai utaita
mashahidi wawili Aprili 24 na mashahidi wengine wawili Aprili 25,2018.
Inadaiwa
kuwa Juni 16, 2008 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido
ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake
vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya
televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya
kupitisha zabuni jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma
na kuinufaisha BVl.
Katika
shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20,
2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa dijitali duniani kati ya
TBC na BVl.
Katika
shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai,
Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa
ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji
kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.
Katika
shtaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido
alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa
kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati
ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Katika
shtaka la mwisho, anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008
akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh887.1 milioni.
Tido anatetewa na Wakili Ramadhani Maleta na yupo nje kwa dhamana.



No comments:
Post a Comment