Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali
imeeleza kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inatekeleza
Mpango wa Miaka Mitano (2017- 2021), wa kusogeza huduma karibu na wateja
kwa kuanzisha ofisi za Kikanda katika Kanda ya Kaskazini, Kusini, Kati,
Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar kwa awamu.
Hayo
yameelezwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu maswali ya msingi ya Mbunge
wa Viti Maalumu Mhe. Jacqueline Msongozi (CCM), aliyetaka kujua lini
Serikali itapeleka Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Ruvuma ili wananchi
waweze kukopeshwa.
Aidha, Mhe. Msongozi alitaka kufahamu utayari wa Serikali kupunguza riba ya mikopo wanayokopeshwa Wakulima katika Benki hiyo.
Akijibu
maswali hayo, Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa hadi kufikia Juni 30,
2018 Ofisi ya Kanda ya Kati, Dodoma, itakuwa imefunguliwa ambayo pia
itakuwa ni Makao Mkauu ya Benki hiyo.
“Baada
ya ufunguzi wa ofisi ya Kanda ya Kati kukamilika Benki Itafanya
uchambuzi wa fursa zilizopo Kikanda na hivyo kuchukua hatua na taratibu
za kufungua ofisi nyingine kulingana na upatikanaji wa rasilimali
fedha”, alisema Dkt. Kijaji.
Alisema
kuwa Benki hiyo inatoa mikopo kwa kutumia mfumo wa makundi, kundi la
kwanza wakulima wadogo wadogo kwa riba ya asilimia 8- 12, kundi la pili
la miradi mikubwa ya kilimo kwa asilimia 12 – 16 kwa mwaka na kundi la
mwisho ni mikopo ya ushirika ambapo riba yake inaendana na hali ya soko
la matumizi ya mkopo.
Kuhusu
kupunguza riba kwa wakopaji, Dkt. Kijaji alibainisha kuwa majadiliano
ya kiwango cha riba yanaweza kufanyika kulingana na historia ya mkopaji.



No comments:
Post a Comment