Mahakama
ya Hakimu Mkazi Iringa imeipiga kalenda kesi ya mwenyekiti wa Mtandao
wa Wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo hadi Jumatatu kutokana na mabishano
makali ya kisheria yaliyotokea kortini hapo kati ya pande mbili za
utetezi na Jamhuri.
Akiahirisha
kesi hiyo, Hakimu Mkazi John Mpitanjia alisema anajipa muda kwa lengo
la kupitia sheria kuhusiana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na
shahidi wa pili; kwamba kielelezo chake kipokelewe na mahakama ama la.
Upande
wa uetetezi ukiongozwa na wakili Jebra Kambole akisaidiwa na Chance
Luwoga, uliomba mahakama kutopokea hati ya upekuzi kwa madai ina
mkanganyiko wa majina na kwamba ni watu wawili tofauti.
Aidha,
utetezi ulipinga hati ya uchunguzi kuwa imekosewa jina la mshitakiwa
kwani badala ya kuandika Abdul Mahamud Omary Nondo imesajiliwa kwa jina
la Mahmud Omary Nondo.
Upande
huo uliomba kutupiliwa mbali kwa nyaraka hiyo ambayo upande wa Jamhuri
ukiongozwa na wakili wa serikali, Alex Mwita akisaidiwa na Pianzia
Nchemba umesema cha muhimu ni ujumbe uliopo ndani.
Mwita alisema huenda nondo alitoa majina mawili tofauli kwa sababu alihojiwa na watu wawili tofauti.
Hoja
ya tatu iliyotolewa na upande wa utetezi ni kwamba ilikuwaje Koplo John
kutumia kifungu cha 10 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai
(CPA)Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kuthibitisha waraka
huo ili hali kabla alisajili kwa kutumia kifungu cha 34 (b) cha Sheria
ya Ushahidi.
Awali,
shahidi wa kwanza ambaye ni E.32328 Koplo Salim aliiambia mahakama
kwamba Nondo aliwasili kituo cha polisi majira ya moja usiku na
kuchukuliwa maelezo ya awali.
Alidai
Nondo alisema amefika kituoni kutoa malalamiko ya kutekwa na watu
wasiojulika na kutelekezwa katika Kiwanda cha Pareto Pct Mafinga.
Kolpo
Salim aliiambia mahakama kuwa Nondo aliiambia Polisi kwamba alitekwa
jijini Dar es Salaam na kusafirishwa hadi Mafinga Iringa na ndipo
alimkabidhi kwa mpelelezi Koplo John mwenye namba E.7665 ambaye ni
shahidi wa pili katika kesi hiyo, ili aweze kumchukua maelezo kwa kina
kuhusiana na malalamiko yake.
Hata
hivyo, mahakama ilipokea vielelezo ambavyo Nondo alivikabidhi Kituo cha
Polisi Mafinga ambavyo ni kompyuta mpakato aina ya Dell, kadi ya
mawasiliano (bussness card), kadi ya benki, simu ya kiganjani aina ya
Itel na kitambulisho cha chuo.
Awali,
Hakimu Mpitanjia alisema kabla ya mashahidi kutoa ushahidi wao inabidi
mtuhumiwa kusomewa mashataka yake yanayomkabili na Nondo alikana
mashtaka hayo.
Jamhuri
imekusudia kuleta mashahidi watano zaidi ambapo jana ni mashahidi
wawili tu waliopanda kizimbani kutokana na kutofikia muafaka baada ya
pande mbili hizo kunyukana kwa kutumia vifungu vya sheria.
Jamhuri
imekusudia kuwaleta pia kutoa ushahidi Koplo Salum, Veronica Fredy
ambaye ni mpenzi wake Nondo, Alphonce Mwamule, Koplo Abdulkadir na mtu
kutoka kampuni ya simu za mkononi ya Tigo.
Nondo
ameshitakiwa kwa makosa mawili ya kuchapisha taarifa za uongo kwa njia
ya kompyuta na kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma ambaye ni
askari polisi Koplo Salim wa Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi.
Ilidaiwa
kwamba Machi 7, mwaka huu akiwa Ubungo jijini Dar es Salaam, mshitakiwa
alitenda kosa la kuchapisha taarifa za uongo kwa njia ya kompyuta
akitumia simu ya kiganjani yenye No. 0659366125 kinyume cha Sheria ya
Makosa ya Mtandao na kusambaza katika mitandao ya kijamii.



No comments:
Post a Comment