Bei
za simu za kisasa nchini zinatarajia kushuka baada ya Tanzania na China
kuingia makubaliano ya ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza simu za
mkononi hapa nchini.
Mbali
na ujenzi wa kiwanda hicho, pia China itajenga kituo cha kutengeneza
program za mawasiliano kwa ajili ya soko la Afrika na Mashariki ya Kati.
Balozi
wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alitoa taarifa hiyo jana
kupitia akaunti ya mtandao wa kijamii wa Tweeter ya Ubalozi wa Tanzania
nchini humo; ambayo ilithibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi
Kasiga.
Aliitaja kampuni itakayotengeneza simu janja (smartphones) kuwa ni Shenzen-Qingchuan Technology (SQTL).
Licha
ya kutokutaja lini uwekezaji huo utaanza na sehemu utakakofanyika,
Balozi Kairuki alieleza kuwa ujio wa kiwanda hicho utafanya bei ya simu
nchini, hususani simu janja kuwa nafuu.
"Kampuni
hiyo imepanga kuwekeza nchini Tanzania kwa kujenga mtambo wa
kutengeneza simu za mkononi pamoja na kituo cha kutengeneza simu za
kisasa za mawasiliano kwa ajili ya soko la Afrika na Mashariki ya Kati,"
alisema balozi Kairuki.
Balozi Kairuki alisema kampuni hiyo ilieleza kuwa itazalisha simu zenye ubora na viwango vya soko la kimataifa.
Alieleza
kuwa Kampuni hiyo pia imepanga kuajiri vijana 100 watakaopelekwa nchini
China katika mji wa Shezen kupata mafunzo kwa muda wa miezi sita.



No comments:
Post a Comment