Rais
John Magufuli jana alishangaa maaskofu nchini kutoa waraka sasa na
akasema hapendi kuuzungumzia bali ataendelea kuisimamamia nchi
aliyokabidhiwa na wananchi.
Rais
Magufuli alishangaa ni kwanini maaskofu hao hawakutoa waraka wakati wa
mauaji ya kinyama ya watu wasio na hatia ya Kibiti mkoani Pwani, na
kuhoji kama marehemu hao walistahili kuuawa.
Kati
ya mwaka 2015-2017, kulikuwa na matukio ya mauaji mfululizo ya watu
zaidi ya 40, wengi wakiwa viongozi na askari polisi mkoani Pwani lakini
sasa yamekomeshwa kwa jitihada za vyombo vya ulinzi na usalama.
Akizungumza
jana wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa usimikaji wa mfumo
wa rada nne za kuongozea ndege jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli
alisema uchumi unakuwa vizuri kutokana na kubana njia zote za wizi wa
mali ya umma uliofanywa na wachache.
"Ninafahamu
hata makanisani zaka zimepungua maana zilikuwa zinatolewa na
mafisadi... Watanzania tusimame twende mbele kwa ajili ya maendeleo
yetu," alisisitiza Rais Magufuli na kueleza zaidi:
"Hakuna waraka uliotoka kwa watu wa Kibiti waliouawa, kwahiyo wao ni sawa kuuawa?
"(Hata hivyo) Sipendi kulizungumzia maana halina msingi... serikali ipo nimekabidhiwa na wananchi kuilinda kwa nguvu zote.
"Wengine nawaangalia, nawachekiii nasema iii," alisema Rais Magufuli na kusababisha mamia ya watu waliohudhuria uzinduzi huo kuangua kicheko.
Aidha, Rais Magufuli alisema kwa miaka mingi nchi imekuwa ikitegemea wafadhili lakini kwa sasa inakwenda vizuri.
"Watanzania
waendelee kuliombea taifa na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo,
napenda mjue kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake
unakwenda mbele," alisema Rais Magufuli.
"Nawaambiwa Watanzania tunaenda pazuri, kazi ya uongozi ni zuri sana... usiposimama na kumtegemea Mungu unaweza kukata tamaa.
"Nawaambia
seriali ipo, haijalala na haitalala, usione simba amelala ukawa
unagusagusa mkia wake. Watanzania tembeeni kifua mbele, tupo pazuri
sana, mtapigwa vita na watu wa nje.
"Tusimame imara, tusonge mbele na tumtangulize Mungu ambaye ni wa kweli kwa watu wa kweli na tutafanikiwa."
Alisema nchi inakwenda vizuri na kutaka Watanzania kutembea kifua mbele kwa kuwa uwezo wa nchi ni mkubwa na wa maajabu na ndiyo maana wenye wivu wanaumia.
Alisema nchi inakwenda vizuri na kutaka Watanzania kutembea kifua mbele kwa kuwa uwezo wa nchi ni mkubwa na wa maajabu na ndiyo maana wenye wivu wanaumia.
"Wenye
wivu wapo sana, hata Mungu aliumba malaika wakatokea mashetani humo
humo, wakagoma, wakatupwa duniani, nao lazima wawe na wivu."
Akidhihirisha
ni jinsi gani nchi inakwenda vizuri, Rais Magufuli alisema kipidi cha
nyuma ilikuwa ni maajabu kwa Tanzania kuonekana angani lakini sasa hivi
heshima yake imerudi.
"Ndege ndiyo heshima ya nchi, tumeingia (madarakani) na kuamua lazima tuwe na ndege zetu na tununue kwa fedha taslimu," alisema.
"Watu
walijiuliza tutapata wapi fedha, nilisema nitawabana mafisadi
watazitema tu na wamezitema na wasiozitema watazitema hata kwa
kutapika."
Alisema
zimenunuliwa ndege sita kwa mpigo bila kukopa kiasi cha dunia kushangaa
na kwamba waliokuwa wanaongeaongea ndiyo wa kwanza kuzipanda.
Tangu
Rais Magufuli aingie madarakani miezi 28 tu iliyopita, nchi ina ndege
tatu mpya aina ya Bombadier Dash 8 Q400 huku tatu nyingine - Bombardier
CS300 kutoka Canada na Boeing 787-8 Dreamliner kutoka Marekani -
zikitarajiwa kufika katikati ya mwaka.
"Tulitakiwa
Watanzania tupendane bila kujali makabila, vyama; mafanikio haya
tuyashangilie, nchi zilizostaarabika duniani masuala ya maendeleo
wanaungana, ndege zikija siyo za familia ya Magufuli ni za Watanzania,
tunajenga vituo vya rada kwa ajili ya Watanzania wote."
Aidha,
Rais Magufuli alisema miradi yote ya maendeleo ni kwa ajili ya
Watanzania na kwamba mawaziri wanapofanya juhudi kubwa, ikiwamo
maboresho ya huduma za afya, huduma ya maji imeongezeka kwa asilimia
14.5 huku mchango wa sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 11.5
hadi 17.5.
Aidha,
alisema ujenzi wa rada za viwanja vya Dar es Salaam, Songwe, Zanzibar,
Mwanza na Kilimanjaro, unatakiwa kukamilika kwa wakati kwa kuwa fedha
zilishatengwa.
"Nakuagiza
Waziri (wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa)
kandarasi wa Mwanza asimamiwe ahakikishe jengo linakamilika," alisema
Rais Magufuli.
"Suala
la fedha serikali ya awamu ya tano haina tatizo na fedha, tena
ulibadili mpangilio wa pa kuanzia, rada zote ziwekwe kwa pamoja."
Aidha, alimwagiza mkandarasi ahakikishe anafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika.
"Waziri usiwe mpole. Nataka uonyeshe ukali wako, kama fedha ni tatizo sema hata leo (jana) utapelekewa, Katibu Mkuu yuko hapa peleka fedha. Asitafute kisingizio cha fedha, zimetengwa bilioni 67.5 kwa ajili ya kazi hii. Uwanja wa Mwanza umesuasua, nataka uwe wa kwanza kukamilika."
"Waziri usiwe mpole. Nataka uonyeshe ukali wako, kama fedha ni tatizo sema hata leo (jana) utapelekewa, Katibu Mkuu yuko hapa peleka fedha. Asitafute kisingizio cha fedha, zimetengwa bilioni 67.5 kwa ajili ya kazi hii. Uwanja wa Mwanza umesuasua, nataka uwe wa kwanza kukamilika."
Awali,
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari,
alisema mamlaka yake imedhamiria kuboresha sekta ya usafiri wa anga na
kuchangia kikamilifu azma ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya
viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Alisema
mradi huo unatarajia kukamilika Mei mwakani ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa vipaumbele vya serikali na TCAA kuimarisha sekta ya
usafiri wa anga.
Hamza
alisema mradi huo utasaidia kurahisisha huduma za utafutaji na uokoaji
kunapotokea ajali za ndege, kuongeza mapato, kuongezeka kwa ndege,
kuiwezesha nchi kukidhi viwango na miongozo ya Shirika la Kimatiafa la
Usafiri wa Anga (ICAO) na kujenga imani ya watumiaji wa anga letu na
kuendana na ushindani katika ukanda wa Afrika na dunia kwa ujumla.
Alisema
TCAA na Kampuni ya M/S Thales Las France SAS ya Ufaransa wameingia
makubaliano ya mradi huo ambao utagharimu Sh. bilioni 76.3 na serikali
itachangia kwa asilimia 100.



No comments:
Post a Comment