KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

September 13, 2018

SERIKALI YAKUSUDIA KUONDOA KODI VIFAA VYA UONGEZAJI THAMANI MADINI

Na Asteria Muhozya, Arusha
Serikali imesema inaangalia uwezekano wa kuondoa kodi ya vifaa vya uongezaji thamani madini  ikilenga kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika nchini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati akijibu swali la mwanafunzi wa Kituo Cha Jemolojia Tanzania (TGC) Rojer Mpele aliyeiomba Serikali kupitia Naibu Waziri kuangalia namna ya kupunguza kodi ya vifaa hivyo ili  kuwasaidia wanafunzi wanaojifunza ukataji na ung’arishaji madini katika kituo hicho kuweza kujiajiri baada ya kuhitimu .

Nyongo ameongeza kuwa, tayari Serikali imeanza kufanya taratibu za kupeleka maombi  kuhusu jambo hilo katika Mamlaka husika ili liweze kufanyiwa kazi kwani litahamaisha uwekezaji wa viwanda vya uongezaji thamani madini nchini ikiwemo kuongeza wigo wa ajira na mapato kupitia sekta ya madini.

Naibu Waziri Nyongo amekitembelea kituo hicho kilichopo jijini Arusha kwa lengo la kujifunza shughuli zinazofanyika kituoni hapo. Kituo cha TGC kipo chini ya Wizara ya Madini, kinatoa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji madini ya vito lengo likiwa ni kuongeza thamani madini.

Ameongeza kuwa suala la uongezaji thamani madini nchini ni jambo ambalo  ni kipaumbele cha serikali kutokana na Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Maboresho yake ya Mwaka 2017 na kwamba tayari serikali imezuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi na badala yake inahamasisha shughuli hizo kufanyika hapa hapa nchini kwa kuwa, zitawezesha kuleta ujuzi, ajira, mapato zaidi ya serikali na kuyaongezea thamani madini hayo nchini kabla hayajasafirishwa nje ya nchi.

“Bado Wizara inaweka msisitizo wa shughuli za uongezaji thamani zifanyike hapa nchini. Kwa hiyo napenda kuwaambia ninyi vijana mnajifunza kitu ambacho ni kipaumbele kwa wizara na serikali,” amesisitiza Naibu Waziri.

Aidha, Naibu Waziri amesema kuwa, serikali kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) unaotekelezwa  chini ya wizara kutokana na mkopo wa Benki ya Dunia, tayari umeagiza vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha karakana ya shughuli za uongezaji thamani madini katika kituo hicho, karakana hiyo inalenga kutumiwa na wahitimu wa kituo husika ili kwawezesha kujiajiri pindi wanapohitimu mafunzo yao.

“Watakaohitimu hapa watalipia gharama ndogo sana za mashine watakazokuwa wakizitumia kufanya kazi zao katika karakana hiyo. Lakini pia, ili kuboresha shughuli za karakana hiyo, tutaendelea kujifunza kwa nchi nyingine namna wanavyoendesha karakana zao,” ameongeza Nyongo.

Katika jitihada za kuendelea kukiboresha kituo husika, Naibu Waziri Nyongo amemtaka Mratibu wa Kituo hicho, kuandaa  Mpango Mkakati wa namna ya kukiboresha na kukitanua kituo hicho ili kiweze kuwa bora na mfano kwa nchi nyingine barani Afrika.

“ Imefika wakati ambapo tunataka TGC kuwa chombo ambacho kinatoa ujuzi wa hali ya juu katika uongezaji thamani madini. Lazima tutoe mafunzo kwa vijana wa kitanzania  na tuendelee kuangalia namna ya kuleta ujuzi au kwa kuwapeleka vijana wetu kujifunza kwa wenzetu na baadaye wawe wakufunzi katika kituo hiki.

Vilevile, Naibu Waziri Nyongo amesisitiza kuwa, Serikali kupitia wizara ya Madini itaendelea kusimamia kwa karibu kuhakikisha kuwa inatekeleza na kutimiza malengo ya uanzishwaji wa kituo hicho. “Lazima ifike mahali kituo kitoe mafunzo kwa jinsi ilivyokusudiwa, ameongeza Nyongo.

Kwa upande wake,  Kaimu Mratibu wa Kituo cha TGC, Eric Mpesa amesema kuwa, kituo hicho ni kituo pekee Afrika Mashariki kinachoendeleza taaluma ya uongezaji thamani madini ya vito na miamba.

Pia, amesema kuwa, kituo kinakusudia kutoa mafunzo ya Diploma ya Gem Jewelly technology ambapo mhitimu katika mwaka wa Kwanza atapatiwa cheti cha NTA Level 4, mwaka wa pili NTA Level 5 na mwaka wa tatu NTA Level 6.

“Kwa kuwa mafunzo yanayotolewa katika kituo hiki ni ya muda mrefu na mfupi, taratibu za kukisajili kwenye Baraza la taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) zilifanywa na kwa sasa kituo kimepata usajili wa kudumu wenye Na. REG/SAT/003,” ameongea Mpesa.

Mpesa ameongeza kuwa, wizara iliamua kuwekeza katika Kituo hicho kwa lengo la kutoa mafunzo ya kuongeza thamani madini ya vito kwa wadau na wajasiliamali wa madini hayo hapa nchini.

Ameongeza kuwa, malengo mengine ni pamoja na kukuza na kuendeleza ujuzi na ufahamu wa kutambua madini ya vito, kuongeza thamani kipato na ajira kwa watanzania.

“ Hivi sasa kituo hicho kinatoa mafunzo ya muda mfupi ya ukataji na unga’rishaji wa madini ya vito na kinaendesha shughuli za uchongaji wa mawe ya miamba kwa kutengeneza  wanyama, ndege, samaki na vitu mbalimbali vya mapambo, amesema Mpesa.

Kituo cha Jemolojia Tanzania (Tanzania Gemological Center -TGC) kilianzishwa mwaka 2003 wakati serikali ikitekeleza mradi wa Maendeleo Sekta ya Madini ( Mineral Sector Development Technical Assistance – MSD TA) ambao ulitekelezwa kati yam waka 1994 na 2005 kwa mkpo kutoka benki ya Dunia. Wakati huo lengo la kuanzissha kituo hicho lilikuwa ni kutekeleza Sera ya Madini ya Mwaka 1997 kuhusu uongezaji thamani madini nchini kwa kuanzia na kutoa mafunzo ya uchongaji wa vinyago vya miamba.

No comments:

Post a Comment