Naibu Waziri wa Fedha,Mwigulu Nchemba |
Dar es Salaam. Watu waliopokea mgawo wa fedha zilizochotwa kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) huenda wakalazimika kulipa mamilioni ya Shilingi ambayo ni kodi ya mapato ya fedha walizopewa, imefahamika.
Hata hivyo, habari zinasema malipo hayo ya kodi
yatafanywa kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi wa vyombo vya dola ambao
unawashirikisha maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu
uhalali wa fedha walizolipwa.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema
juzi kuwa wote waliopokea mgawo wa fedha zilizochotwa kutoka katika
akaunti hiyo watapewa fomu za kuthibitisha mapato yao ili wakatwe kodi
kutokana na fedha hizo ambazo pia zinapaswa kuhakikiwa na vyombo vya
usalama kwamba ni mapato halali.
Alisema taratibu za kufuatilia fedha hizo
zimekwishaanza na ifikapo Desemba 31 wahusika watapewa fomu ili
kuthibitisha mapato yao ili hatua za kuwatoza kodi zianze.
Msingi wa maelezo ya Nchemba umejengwa kwenye
Sheria ya Mapato ya Kodi (Income Tax Act) ya 2012 ambayo inaelekeza
mlipaji wa kodi kuwasilisha ankara za hesabu za mapato yake kwa TRA kila
ifikapo mwisho wa mwaka na hesabu hizo huiwezesha mamlaka hiyo
kutathmini kiwango cha kodi inayopaswa kulipwa na mhusika.
“Hotuba ya Rais (Jakaya Kikwete) imetupa nguvu
kuendelea na juhudi ambazo tayari tulikwishazianza tangu awali, maana
amesisitiza kwamba lazima kodi ilipwe na sisi hilo ni jukumu letu,
tutafuatilia ili kuhakikisha kwamba fedha za walipakodi zinarejeshwa,”
alisema Nchemba.
Ikiwa wote waliotajwa watalazimika kukatwa
asilimia 30 ya fedha walizopewa kama kodi ya mapato, TRA itakusanya
zaidi ya Sh9.3 bilioni ambazo zinatokana na karibu Sh31 bilioni
zilizotawanywa kwa watu na kampuni mbalimbali kutoka kwenye akaunti ya
mmiliki wa VIP Engineering, James Rugemalira.
Miongoni mwa waliokiri kupokea fedha hizo ni
aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka ambaye alipata mgawo wa Sh1.6 bilioni akisema fedha hizo
zilikuwa ni za mchango wa kulipa mkopo wa shule anayoisimamia.
Hata hivyo, hatua yake hiyo tayari imemgharimu
baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uwaziri wake kutokana na kile
alichokiita kuwapo kwa makosa ya kimaadili hasa ikizingatiwa kuwa fedha
hizo ziliingizwa kwenye akaunti yake binafsi.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment