Lowassa |
Utafiti
uliofanywa na Taasisi ya Positive Thinkers Tanzania (PTT), umeonyesha
kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, anaongoza kati ya wanaotajwa
kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Utafiti huo pia unamuweka Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa katika nafasi ya pili.
Matokeo ya utafiti huo yamewapa nafasi za juu wanasiasa hao baada
ya utafiti wa Shirika lisilo lwa kiserikali la Twaweza mwaka jana kumpa
Lowassa nafasi ya kwanza na Dk. Slaa nafasi ya tatu.
Utafiti wa PTT yenye makao makuu jijini Dar es Salaam, matokeo yake
yaliyotangazwa jana yanaonyesha kuwa Lowassa alipata kura 752 kati ya
3,298 zilizopigwa.
Dk. Slaa alipata kura 644 na Naibu wa Fedha, Mwigulu Nchemba 350.
Akitangaza ripoti ya utafiti huo jijini Dar es Salaam, Rais wa
Taasisi hiyo, Tibatizibwa Gulayi, alisema ulifanywa katika mikoa 13 kwa
kuwauliza wananchi kwa njia ya madodoso kisha taarifa zake kuingizwa
katika mfumo wa Elektroniki unaojulikana kama Fast web application
system (FWAS).
Alisema kuwa utafiti huo ulianza Februari, mwaka huu na kumalizika
mwanzoni mwa Machi, mwaka huu na ulihusisha majina wanasiasa 15
wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini.
Gulayi alisema wanasiasa wengine waliotajwa na kura zao kwenye
mabano ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba
(294); Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (227); Kiongozi Mkuu wa ACT –
Tanzania, Zitto Kabwe (224); Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe (197); Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (107) na
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta (72).
Wengine ni Naibu waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba (54); Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum),
Profesa Mark Mwandosya (40); Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
(34) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi
(31).
Waliofuatia ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira (16) na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye (10).
Watu ambao walisema hawana mgombea walikuwa 79 wakati waliosema mgombea yeyote atakayegombea ni sawa walikuwa 167.
No comments:
Post a Comment