Kada aliyewania ubunge kupitia Chadema katika Jimbo la Kalenga
na kutemwa kwenye kura za maoni, Mwanahamisi Muyinga ameibuka mshindi wa
kura hizo katika jimbo hilohilo kupitia chama cha ACT-Wazalendo.
Katika uchaguzi uliofanyika katika Kata ya Mlandege mwishoni mwa wiki iliyopita, Muyinga aliibuka mshindi kwa kupata kura 10 akifuatiwa na Daniel Mwangili aliyepata kura saba, huku Edward Mtakimwa na Kiduo Mgunga wakipata kura tatu kila mmoja.
Mbali na Muyinga, wengine waliotemwa Chadema na kushinda ACT ni aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kunduchi, Janeth Rithe na Dickson Ngh’illy aliyewahi kugombea Jimbo la Temeke mwaka 2010. Ofisa wa Habari wa ACT- Wazalendo, Abdallah Khamis alisema jana kuwa Ngh’illy ameshinda katika jimbo jipya la Kibamba baada ya kupata kura 19 kati ya 29 zilizopigwa.
Alisema kabla ya kura hizo kupigwa, mgombea mmoja alijitoa na kuacha nafasi hiyo ikiwaniwa na Ngh’illy, Monalisa Ndala na Edna Mwango aliyeambulia kura mbili. “Rithe ameshinda baada ya kupata kura 38 kati ya 58 Jimbo la Kawe, huku Mohamed Ngulangwa akiibuka kidedea Jimbo la Temeke baada ya kupata kura 80 kati ya 93,” alisema Khamis.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Muyinga aliwashukukuru wapigakura na wakazi wa Kalenga kwa kumuamini na kumpa fursa ya kupeperusha bendera ya chama hicho na kwamba hatawaangusha.
“Nawashukuru kwa kunipa heshima hii. Nataka kuwaeleza kuwa mimi natoka ukoo wa machifu, nimeomba ruhusa ya kuifanya kazi hii katika Jimbo la Kalenga na nimeruhusiwa,” alisema Muyinga na kuongeza:
“Nawafahamu wakazi wa Kalenga kwa zaidi ya asilimia ya 90. Najua kuwa wanategemea kilimo na mimi nimesoma mambo ya kilimo, nitatumia taaluma yangu kuwaletea maendeleo.”
Mwananchi.
No comments:
Post a Comment