Mkuu wa Huduma za matawi Benki
ya Exim Tanzania, Bw Eugine Massawe (kulia) pamoja na Meneja Mkuu wa
kampuni ya Pacific International Lines, PIL Bw. Kevin Stone wakikata
utepe kuashiria uzinduzi wa mashine ya kuweka pesa (CDM) ya benki hiyo
itakayowawezesha wateja wa kampuni ya PIL kuweka pesa kwenye akaunti zao
moja kwa moja bila kulazimika kufika kwenye ofisi au kuhudumiwa na
wafanyakazi wa benki hiyo.
……………………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu
BENKI ya Exim Tanzania imezindua
mashine yake ya kwanza ya kuweka pesa (CDM) itakayowawezesha wateja wa
kampuni ya Pacific International Lines, PIL kuweka pesa kwenye akaunti
zao moja kwa moja bila kulazimika kufika kwenye ofisi au kuhudumiwa na
wafanyakazi wa benki hiyo.
Ufunguzi wa mashine hiyo
ulifanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni ukihusisha mwakilishi wa
benki hiyo ambaye ni Mkuu wa Huduma za matawi Bw Eugine Massawe pamoja
na Meneja Mkuu wa kampuni ya PIL Bw. Kevin Stone.
Akizungumzia mashine hiyo iliyopo
kwenye jengo la Maktaba (Makataba Square)lililopo katikati ya jiji, Bw
Massawe alisema ni mwendelezo wa mkakati wa benki hiyo katika
kurahisisha huduma zaidi za kifedha kwa wateja wa benki hiyo.
“Mashine hii itawawezesha wateja
wetu kuweka pesa moja kwa moja kwenye akaunti zao wao wenyewe. Huduma
hii itapatikana kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 na nusu jioni kila
siku na itatoa fursa kwa wateja wa PIL kupata msaada kutoka kwa
wahudumu wetu waliopo jirani na mashine pale watakapohitaji,’’ alisema
Kwa mujibu wa Bw Massawe, kwa
kuanzia mashine hiyo itaanza kupokea noti za Dola ya Kimarekani kwa
kiasi chochote huku akitahadharisha; “Ifahamike kwamba mashine hii ina
uwezo mkubwa wa kutambua pesa bandia au zile zisizofaa kwa kuwa
imewekewa mfumo bora kabisa wa kiusalama,”
Aliongeza kuwa mashine hiyo
inamuwezesha mtumiaji kupata risiti ya muhamala atakaoufanya sambamba
na kumuhakikishia mafanikio ya muhamala husika.
“Mteja atapokea ujumbe mfupi wa
maneno kuhusiana na mwenendo ya muhamala alioufanya,’’ alisema Bw
Massawe huku akisisitiza: “Benki ya Exim itabaki kuwa benki pekee yenye
kubuni huduma zinazokidhi matakwa ya wateja kulingana na mabadiliko ya
kimahitaji katika huduma za kibenki,’’
Alisema huduma hiyo imewekwa
jirani na makao makuu ya benki hiyo ili kuwawezesha watumiaji wa huduma
hiyo kupata msaada kwa urahisi kutoka kwa wafanyakazi wa benki pale
wanapohitaji.
“Itakapofikia kipindi ambacho
wateja wetu watakuwa tayari wamejenga uelewa wa kutosha kuhusiana na
matumizi sahihi ya mashine hii tutakuwa tayari kuongeza mashine nyingine
katika maeneo mbalimbali ili waweze kufurahia huduma hii zaidi,’’
aliahidi.
|
April 27, 2016
BENKI YA EXIM YAZINDUA MASHINE YAKE YA KWANZA YA KUWEKA PESA KWENYE AKAUNTI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment