NA MWANDISHI WETU
SHIRIKISHO la Riadha la
Kimataifa (IAAF), limemteua Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT),
Anthony Mtaka, kuwa miongoni mwa wajumbe wanaounda kundi la ushauri wa
mikakati ya mawasiliano ya shirikisho hilo.
Rais wa IAAAF ,Lord Sebastian Coe alitangaza uteuzi huo hivi
karibuni ambapo wajumbe wengine ni Abrahamson Alan wa Marekani, Rodan
Joe Junior ,Sierra Calixto ,,Karamarinov Dobromir kutoka Bulgaria
na Rochdi Souad wa Ufaransa.
Akizungumza kuhusu uteuzi huo Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa mkoa
wa Simiyu, alisema amepokea uteuzi huo kwa furaha kutokana na kuwa ni
nafasi ya juu ktk sekta maarufu ya michezo katika ngazi ya kimataifa.
“Nimefurahishwa na uteuzi huu hasa ukizingatia nimeteuliwa
nikiwa rais wa shirikisho la riadha mwenye umri mdogo kuliko wote kwa
sasa atakuwa na fursa ya kujifunza mambo mengi mazuri.”alisema Mtaka.
Alisema uteuzi huo ni faida kubwa kwa maendeleo ya michezo
katika taifa letu, hasa kipindi hiki ambapo serikali ya awamu ya tano
inapoandaa mkakati wa kuiweka sekta ya michezo kuwa sehemu kubwa ya
ajira.
Mtaka alisema Tanzania itapata nafasi pana zaidi ya kuwakilishwa
katika mikutano mikubwa ya mchezo wa riadha duniani (Decision Making)
eneo ambalo linatoa fursa kubwa kwa maandalizi ya mashindano makubwa
yajayo baada ya mashindano ya Olyimpiki yatakayofanyika katika jiji la
Rio de Jeneiro mwaka huu.
“Taifa litarajie uwakilishi
wenye tija, sababu mimi nimeteuliwa kati ya wajumbe nane ambao kila
mmoja wao anawakilisha eneo kubwa, hivyo kama nimepewa dhamana ya
kuiwakilisha bara zima la Africa, kwa vyovyote nitaweka maslahi ya nchi
yangu mbele bila kuathiri utendaji wa jukumu nililopewa.”alisema Mtaka.
“ Uteuzi wangu ni sifa kwa
taifa zima, sifa ambayo itafufua mtazamo mwema ulioonyeshwa na
wanariadha wakongwe walioiletea taifa sifa kama Filbert Bayi, Suleiman
Nyambui, Gidamis Shahanga, Juma Ikangaa bila kumsahau Mzee John Stephen
Akhwari aliyeshiriki Mexico City Games 1968.”aliongeza Mtaka.
Aidha Mtaka alisema uteuzi huo umeongeza hamasa ya kuwekeza
maradufu katika kambi ya timu ya taifa ya riadha iliyopo katika hosteli
ya Chuo cha misitu cha FITI kilichopo West Kilimanjaro wilayani Siha na
Arusha.
No comments:
Post a Comment