Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga, akitoa
ufafanuzi kuhusu stika za upimaji uzito katika mizani kwa magari
makubwa yanayosafiri kwenda nje ya nchi.
………………………………………………………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng.Joseph Nyamhanga
ametambulisha utaratibu mpya utakaotumika kupunguza vikwazo visivyo vya
kiforodha ili kurahisisha biashara na usafirishaji kwa magari makubwa
yanayosafiri kwenda nje ya nchi.
Utaratibu huo unaotarajiwa kuanza
Mei mwaka huu utawezesha magari yanayosafiri nje ya nchi kukagulia
katika vituo visivyozidi vinne ili kupunguza muda wa safari kwa magari
yaendayo nje ya nchi na kuvutia wasafirishaji kutumia bandari ya Dar es
Salaam.
“Tumetayarisha stika
zitakazobandikwa kwenye magari yanayokwenda nje ya nchi ambayo
yatasimama na kukaguliwa katika vituo vitatu kwa magari yanayotumia
barabara ya kanda ya kati na vinne kwa yanayotumia kanda ya Dar es
salaam yaani TANZAM ”amesema Eng. Nyamhanga.
Eng. Nyamhanga amevitaja vituo
hivyo vya barabara ya ukanda wa kati kuwa ni Vigwaza mkoani Pwani,
Manyoni mkoani Singida na Nyakanazi mkoani Kagera na kwa ukanda wa Dar
es salaam yaani barabara kuu ya TANZAM- Dar es salaam hadi Tunduma na
Uyole hadi Kasumulu vitatumika vituo vine ambavyo ni Vigwaza mkoani
Pwani,Mikumi mkoani Morogoro, Makambako mkoani Njombe na Mpemba mkoani
Songwe.
Vituo hivyo vya ukaguzi wa pamoja
vitakuwa na huduma ya Mizani, Vituo vya Polisi, Mamalaka ya Mapato
Tanzania (TRA), na maeneo ya kupumzikia madereva wanaosafiri kwenda nje
ya nchi.
Katika hatua nyingine Eng.
Nyamhanga amesema ili kurahisisha biashara ya usafirishaji kati ya
Tanzania na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC), na Jumuiya ya Soko la Pamoja kwa
Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) Serikali inaendelea
kutoa huduma za pamoja mipakani one stop border post
inayolenga kurahisisha huduma za forodha,uhamiaji na usimamizi wa ubora
wa bidhaa na huduma ,ulinzi na usalama kwa kutoa huduma hizo upande
mmoja wa mpaka kwa nchi mbili husika.
Vituo hivyo vinavyojengwa katika
mipaka ya Holili, Namanga, Horohoro,Sirari, Mtukula, Rusumo, Kabanga,
Tunduma na Kasumulu vitaimarisha huduma za forodha,uhamiaji ulinzi na
usalama.
|
No comments:
Post a Comment