Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Shirikisho la Muziki Tanzania
limewataka wananchi kuwapuuza wanamuziki wasio na maadili ili kuondokana
na mmomonyoko wa maadili unaosababishwa na shughuli zao za kimuziki.
Tamko hilo limetolewa leo Jijini
Dar es Saalam na Rais wa Shirikisho hilo, Addo November alipokua
akimtambulisha Katibu Mkuu wa Shirikisho la muziki ambaye ni John
Kitime.
“Mchakato wa kumtafuta Katibu
Mkuu tumeufanya bila kukurupuka, nimefarijika sana kwa kukubali kwake
ili kuhakikisha tunawakwamua wanamuziki kwasababu changamoto za muziki
tulizokuwa nazo ni nyingi ikiwemo ya wanamuziki wasio na maadili”,
alisema November.
November aliongeza kuwa
changamoto kubwa ni Sheria mbovu ya Haki Miliki ambayo mchakato wa
kuirekebisha sheria hiyo pamoja na marekebisho ya sera ya utamaduni upo
katika hatua za mwisho pia shirikisho limefanya jitihada za kuweka
kipengele kinachozungumzia masuala ya sanaa kama haki ya msingi katika
mchakato wa katiba mpya.
Aidha, alisisitiza kuwa
shirikisho hilo halipo kwa kumsaidia mwanamuziki mmoja mmoja bali ni
kuhakikisha mfumo mzima wa muziki nchini unaweza kuwanasua wanamuziki
wote na tasnia kiujumla ili muziki uwe na heshima.
Naye, Katibu Mkuu mpya wa
Shirikisho hilo, John Kitime amesema kuwa anategemea kutoa elimu kwa
wanamuziki kuhusu kazi zao kupitia semina mbalimbali pamoja na
kuimarisha shirikisho hilo ili vikundi vya wanamuziki viweze kusimama
na kukuza muziki ili iwanufaishe wanamuziki wenyewe.
“Sheria ya Haki za Binadamu namba
245 iko wazi kuwa kila mtu anastahili kupata mafao yake yanayotokana na
ubunifu wake kwahiyo kutowalipa ni kuvunja haki hiyo ya binadamu, kazi
kubwa tuliyonayo ni kuwaelimisha wanamuziki kufahamu haki zao”, alisema
Kitime.
Shirikisho la Muziki Tanzania
linajumuisha mwanamuziki mmoja mmoja pamoja na vikundi ambalo limeundwa
na vyama 7 ambavyo vimesajiliwa na Baraza la Sanaa Tanzania vifuatavyo;
Chama cha Muziki wa Taarabu, Chama cha Muziki wa Rhumba, Chama cha
Muziki wa Dansi, Chama cha Muziki wa Asili, Chama cha Muziki cha Wapiga
Muziki wa Diski, Chama cha Muziki wa Kizazi kipya pamoja Chama cha
Muziki wa Injili.
|
June 3, 2016
SHIMUTA WATAKA WANAMUZIKI WASIO NA MAADILI KUPUUZWA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment