WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Dodoma pamoja na
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kutenga eneo la bandari kavu
ili mkoa huo uweze kupokea na kuhifadhi mizigo na kurahisisha biashara
kwa mikoa jirani.
Ametoa
agizo hilo jana jioni (Jumatano, Julai 20, 2016) wakati akizungumza na
mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma mara baada ya kuweka jiwe la msingi
kuashiria uzinduzi wa awamu ya kwanza ya ukarabati na upanuzi wa uwanja
wa ndege wa Dodoma.
“Ninazo
taarifa kuwa Benki ya Dunia kupitia shirika la Local Investment Climate
(LIC) tayari wametenga fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili
ya kujenga bandari kavu na tayari fedha hizo zimeshapokelewa na Mkoa wa
Dodoma kwa ajili ya kazi hiyo.”
“Uzuri
wa mkoa wa Dodoma kuna reli. Kwa hiyo makontena yanayoenda Burundi na
mahali kwingine yatashushwa hapa na kukaa kwenye bandari kavu; hivyo,
wafanyabiashara watachukua mizigo yao hapa badala ya kupata shida ya
kuyafuata Dar es Salaam kama ilivyo sasa,” amesema.
Waziri
Mkuu ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itoe wataalam
ili washirikiane na CDA kufanikisha kazi hiyo. Amesema hatua hiyo
itasaidia kurahisisha wananchi na wafanyabiashara kupata huduma hiyo kwa
urahisi na umbali mfupi tofauti na hali ilivyo sasa.
Ameuagiza
pia uongozi wa CDA utenge eneo maalum la kituo cha biashara (commercial
hub)) ili Kanda zote zinazozunguka mkoa wa Dodoma na nchi jirani wapate
bidhaa mbalimbali kutokea Dodoma.
“Kutokana
na upanuzi huu na fursa zinazojitokeza, hii iende sambamba na
kuwatengea maeneo maalum wajasiriamali badala ya kuwaacha kuzagaa kila
mahali,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Akizungumzia
kuhusu upanuzi wa uwanja huo, Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa mradi
huo kutaziwezesha ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 90 zianze kutua
kwenye kiwanja hicho na kukuza fursa za kibiashara zinazohitaji usafiri
wa haraka na salama.
“Katika
Ilani ya CCM, suala la ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja
vya ndege limepewa umuhimu mkubwa sana na ndiyo maana leo tunashuhudia
utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais ambaye amewezesha upatikanaji wa
fedha za ukarabati na fidia kwa wananchi wa kata za Makole na Uwanja wa
Ndege ambao maeneo yao yametwaliwa na Serikali ili kufanikisha upanuzi
huu,” amesema.
Amesema
uzinduzi huo ni mwanzo tu wa utekelezaji wa miradi mingine ya kuboresha
na kupanua viwanja vya ndege nchini ambapo Serikali kwa kutumia vyanzo
vyake vya mapato ya ndani na ya nje, itaendelea kuboresha zaidi
miundombinu na huduma nyingine za viwanja vya ndege kama vile Mtwara na
Mwanza ambavyo amesema vitapanuliwa kufikia hadhi ya kimataifa.
Ameitaja
miradi mingine kuwa ni viwanja vya ndege vya Kigoma na Tabora ambavyo
vinaendelea kupanuliwa kwa kujenga majengo ya abiria na maegesho ya
ndege ili kufikia viwango vya huduma za kimkoa; viwanja vya Shinyanga na
Sumbawanga vitapanuliwa kwa kuboreshwa miundombinu na majengo yake
kufikia hadhi ya viwanja vya kimkoa; huku kiwanja cha ndege cha Lindi
kikiboreshwa miundombinu yake kufikia hadhi ya kimkoa na kuweza
kuhudumia viwanda vinavyotokana na uchumi wa mafuta na gesi.
Amesema
Serikali itaendelea kukamilisha ujenzi wa jengo la tatu la abiria
(Terminal 3) katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA) ambalo likishakamilika Desemba 2017 litahudumia abiria wapatao
milioni 6 kwa mwaka; ilhali kiwanja cha ndege cha kimataifa cha
Kilimanjaro (KIA) kinapanuliwa miundombinu yake na jengo la abiria ili
kiweze kuhudumia abiria milioni 1.2 kwa mwaka.
Akimkaribisha
Waziri Mkuu kuhutubia hadhara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa ameiomba Serikali iendelee kuwekeza
katika ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato ili ndege za kimataifa
ziweze kutua kwenye mkoa huo.
Mapema,
akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Dk. Leonard Chamuriho amesema Serikali imetoa
sh. bilioni 11.8 kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba hadi sasa
wamekamilisha asilimia 60 ya ujenzi kwa kuweka lami umbali wa km.2.0
kati ya km.2.5 zinazohitaji kukamilishwa chini ya mradi huo.
Amesema
hivi sasa ndege zinazoweza kuruka na kutua kwa umbali huo zinaweza
kuanza kutoa huduma kwenye uwanja huo wakati wakiendelea kukamilisha
ujenzi wa mita 500 zilizobakia.
No comments:
Post a Comment