Na Ramadhan Ali/Maelezo Zanzibar
Mtaalamu wa Sayansi ya ganzi na
usingiza Dkt. Lee Ngungi kutoka Kenya amesema teknolojia ya taaluma
hiyo inabadilika kwa haraka hivyo kuna haja kwa madaktari
wanaoshughulika na fani hiyo kuandaliwa mafunzo ya mara kwa mara ili
kwenda sambamba na mabadiliko hayo duniani.
Dkt. Ngungi ambae alikuwa
mkufunzi wa mafunzo ya siku tatu ya madaktari wa ganzi na usingizi wa
Zanzibar yaliyofadhiliwa na Jumuia ya Kanga Maternity Trust katika
Hoteli ya Mazsons Shangani, amesema elimu kwa ajili ya madaktari wa kada
hiyo inahitaji kupewa kipaumbele ili kuwajengea uwezo wa kuhudumia
jamii kwa ufanisi zaidi.
Amesema lengo la teknolojia ya
ganzi na usingizi kwa sasa hasa kwa upande wa mama wajawazito inapobidi
kufanyiwa upasuaji ni kuwawezesha kujifungua bila matatizo na baada ya
kupata fahamu wasiweze kupata maumivu makali.
Dkt. Ngungi amezishauri jamii za
nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki kuunga mkono na kuthamini juhudi
zinazochukuliwa na Serikali na Taasisi nyengine za Kimataifa na Kitaifa
za kuwapatia elimu madaktari wa ganzi na usingizi katika nchi zao.
Mratibu wa mafunzo hayo ambae ni
Mkuu wa Kitengo cha ganzi na usingizi katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja
Dkt. Khamis Wazir amesema mafunzo hayo ya kwanza, ndani ya kazi, kwa
wafanyakazi wa kada hiyo Zanzibar yataongeza ufanisi katika kuhudumia
mama wajawazito.
Ameishukuru Kanga Maternity Trust
kwa kushirikiana na Hospitali kuu ya Mnazimmoja kufadhili mafunzo hayo
na kusema kuwa wataalamu wa fani ya ganzi na usingizi wanahitaji vifaa
na elimu zaidi ili kupunguza vifo vya mama wajawazito wakati wa
kujifungua.
No comments:
Post a Comment