KATIBU Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, atatua ofisini kwa kiongozi
mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, ili kumueleza
mkakati wake wa kutua ofisini kwake, Buguruni jijini Dar es Salaam, anaandika Pendo Omary.
Maalim anakwenda kwa IGP Mangu kumueleza adhima yake ya kufika ofisi kuu ya chama chake kesho Ijumaa, majira ya saa mbili asubuhi.
Hatua ya Maalim kutinga ofisini kwa IGP imetokana na kitendo
cha jeshi la polisi kumsindikiza Prof. Lipumba kurejea ofisini; kusaidia
uharibifu wa mali na kushambulia wanachama na wafuasi wa chama hicho.
Azma yake ya kwenda ofisini kwake kesho, inatokana na ofisi hiyo
kuvamiwa na aliyepata kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim
Lipumba na genge la wafuasi wake.
Prof. Lipumba aliyejiuzulu uenyekiti wa CUF, 6 Agosti mwaka jana na
miezi 11 baadaye akatangaza kurejea katika nafasi yake, amefukuzwa rasmi
uanachama wa chama hicho Jumanne iliyopita na Baraza Kuu la uongozi la
Taifa (BKT), lililokutana Visiwani.
Hata hivyo, Prof. Lipumba, ameendelea kung’ang’ania kuwa bado
mwenyekiti halali wa chama hicho na msimamo wake huo, unadaiwa kuungwa
mkono na msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa watu waliokaribu na Maalim Seif
zinasema, kiongozi huyo amekwenda kwa IGP Mangu kumtaarifu kuwa yeye na
wabunge wa chama hicho, wamepanga kufika Buguruni kwa pamoja.
Anasema, “Maalim Seif anakwenda kumweleza IGP Mangu kwamba, tayari
kumekuwepo na viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na watu wa
Prof. Lipumba na kwamba chochote kitakachotokea, yeye na jeshi lake,
wanapaswa kubeba msalaba.”
Prof. Lipumba alijiuzulu uenyekiti karibu na uchaguzi mkuu mwaka
jana, akakimbilia nje ya nchi huku akidai hakufurahishwa na Edward
Lowassa kuwa mgombea urais chini ya mwavuli wa vyama vinne ikiwamo CUF.
Ukawa unaundwa na vyama vinne; Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na National League for Democrats (NLD).
Hii ni mara ya pili tangu mfumo wa vyama vingi urejee nchini, kukumbwa na “mbegu mbaya” ndani yake.
Mara ya kwanza ilikuwa pale Augustine Mrema, akiwa mwenyekiti,
alipojiapiza kufukuza wanachama thabiti ndani ya NCCR-Mageuzi.
Alishindwa. Alifukuzwa mwenyewe.HISANI YA MWANAHALISI ONLINE
No comments:
Post a Comment