-Aeleza siri ya mafanikio ya kampuni ya TBL Group
 Mkurugenzi wa ufundi wa TBL Group na viwanda vya SABMiller kanda ya Afrika Mashariki,Gavin Van Wijk,amesema mkakati wa serikali ya awamu ya tano wa kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda unaweza kutekelezeka na kuleta maendeleo makubwa kwa nchi.
Alisema kinachotakiwa kufanyika haraka ni kujifunza kutoka nchi zilizofanikiwa katika sekta ya viwanda na kutumia mifumo ya uendeshaji viwanda kwa tija na ufanisi inayotumika katika nchi hizo ambayo imeziwezesha kuwa na viwanda imara.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam jana,Wijk alisema kampuni ya TBL Group imeanza kuonyesha njia kuwa Tanzania ya viwanda inawezekana kutokana na viwanda vyake vya kutengeneza bia vilivopo nchini kuwa miongoni mwa viwanda bora vinavyoongoza barani Afrika kwenye mtandao wa viwanda vilivyopo chini ya kampuni ya SABMiller.
“Kwa miaka 6 mfululizo viwanda vya Tanzania vimekuwa vikishinda tuzo mbalimbali za ubora na kuwa tishio kwa viwanda vingine vilivyopo kwenye nchi nyinginezo  za Afrika na mwaka huu rekodi ya kiwanda bora barani Afrika inashikiliwa na kiwanda cha TBL Mbeya  wakati nafasi ya pili inashikiliwa na kiwanda cha Mwanza pia viwanda vya Arusha navyo viko kwenye nafasi za juu na bidhaa zinazotengenezwa na viwanda hivi ni tishio katika masoko ya kimataifa”.Alisema.
wijk-2
Mkurugenzi wa Ufundi wa TBL Group, Givan Van Wijk akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kushoto kwake ni Maofisa Waandamizi wa kampuni hiyo.
Alisema siri ya mafanikio haya ni kuhakikisha mifumo ya kampuni ya uzalishaji wenye tija inafuatwa  na matokeo yake ni kupatikana kwa uzalishaji wenye tija na viwango vya kimataifa.”TBL Group tunatekeleza programu ya uendeshaji viwanda kwa ufanisi ya kampuni ya SABMiller inayojulikana kama Manufacturing Way ambayo ikitekelezwa ipasavyo popote pale lazima ufanisi upatikane”.Aliseme Wjik.
Aliongeza kuwa inafurahisha kuona watanzania wapo makini kujifunza Programu mbalimbali za kuleta ufanisi na kuzitekeleza kwa umakini mkubwa na kuwa  viwanda vya TBL Group ambavyo vinazidi kuwa tishio kwa ubora barani Afrika na sehemu nyinginezo duniani  vinaongozwa na watanzania na wafanyakazi katika viwanda hivi ni watanzania wenyewe.
 Alisema mafanikio mengine kwa viwanda hivi yanatokana pia na uwekezaji unaofanyika kila mwaka kwenye mitambo na vitendea kazi vya kisasa ambapo kampuni inatumia zaidi ya dola milioni 14 katika uwekezaji wa kufunga za kisasa,uwekezaji ambao pia  unaenda sambamba na kuwekeza kwa mafunzo ya wafanyakazi ili waweze kuitumia kuleta ufanisi.”Tumekuwa tukiendesha mafunzo ya ndani na nje kwa wafanyakazi wetu wote mara kwa mara kwa ajili ya kuwawezesha kwenda sambamba na mifumo ya kimataifa ya uzalishaji wenye tija kwenye viwanda vyetu”.Alisisitiza Wijk.
 Mafunzo wanaoyapata wafanyakazi mbali na kuwasaidia kuleta ufanisi katika kazi zao viwandani alisema pia yanawasaidia wanapokuwa nje ya kazi za ofisi.Alitoa mfano kuwa wafanyakazi wanafundishwa kufuata ratiba katika utekelezaji wa  shughuli zao za kila siku,kuzingatia muda,usafi wa mazingira,  kuzingatia usalama kwa kwao binafsi na  watu wengine,umuhimu wa kufanya mazoezi na mambo mengineyo mengi.
wijk-3
Pia alisema  kampuni inatekeleza malengo ya SABMiller  ya ustawishaji jamii na kuleta maendeleo endelevu ambayo yanashabiana na malengo ya Umoja Wa Mataifa na utekelezaji wake umeonyesha kuleta manufaa katika sehemu zote ambako viwanda vya kampuni  vilipo.
Baadhi ya malengo aliyataja kuwa yamelenga kutunza mazingira na vyanzo vya maji,kuwezesha wazalishaji wanaouzia kampuni malighafi,kuongeza fursa za ajira za moja kwa moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja “Kampuni imepata mafanikio kwa kuwezesha wakulima wanaouzia malighafi kupitia mpango unaojulikana kama Go Farming ambao unaendelea kubadilisha maisha ya wakulima kuwa bora.Tumeanza na wakulima wa Shahiri na Zabibu  na tutahakikisha mpango huu unawafikia wakulima wengi zaidi nchini”.Alisisitiza.
Kuhusiana na suala la Usalama alisema kuwa limekuwa likipewa kipaumbele katika viwanda vyake vyote na kutokana na wafanyakazi kupatiwa mafunzo ya usalama mara kwa mara matukio ya ajali yamepungua kwa kiasi kikubwa ni nadra kutokea pia usalama hauishii kwa wafanyakazi pekee bali hata kwa wakandarasi wanaofanya kazi viwandani na kwa wageni wanaotembea viwanda.“Kwenye suala la usalama tumekuwa tukishinda tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo ya Usalama mahali pa kazi ya OSHA na tuzo ya usalama wa viwandani ya kimataifa ijulikanayo kama NOSA kwa kiwango cha Nyota 5.
wijk-7
Mkurugenzi wa Ufundi wa TBL Group,Givan Van Wijk (kulia) katika picha ya pamoja na baadhi ya Maofisa Waandamizi wa kampuni hiyo.
 Motisha kwa wafanyakazi alisema ni moja ya suala ambalo kampuni imekuwa ikilipa umuhimu mkubwa  “Motisha hizi zimetuwezesha kupata mafanikio makubwa na zimepelekea kampuni kushinda tuzo ya Mwajiri bora inayotolewa na Chama Cha Waajiri Nchini (ATE) na tuzo ya mzalishaji bora inayotolewa na Shirikisho la Viwanda Tanzania”.
Alimalizia kwa kusema kuwa kampuni itaendelea kubuni mikakati ya kuendelea kufanya vizuri katika uzalishaji na kwenye masoko  na kuhakikisha uwekezaji wake unaleta manufaa kwa taifa kuanzia kwenye kuchangia pato la serikali kwa njia ya kulipa kodi na kuleta mabadiliko  kwenye jamii pia  kufungua milango kwa viwanda na taasisi nyingine zinazotaka kujifunza mifumo ya uendeshaji viwanda kwa kufuata mifumo yenye kuleta tija na ufanisi.