Prof. Tibaijuka ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya tuzo ya kimataifa ya Mwanamfalme Khalifa bin Salman Al Khalifa aliyoipata hivi karibuni.
“Nilipewa tuzo ya dola laki moja ambayo sikuichukua kwa sababu ya yaliyonikuta hapa nchini, hata wahusika niliwaambia kuwa sheria ya nyumbani hairuhusu watumishi kupokea tuzo ya fedha na kwamba niliwarudishia ili waitumie hiyo fedha wanavyotaka, ” amesema.
Amesema kuwa kama wahusika wataipeleka fedha hiyo mkoani kwake Kagera ambapo wananchi wake wamepata maafa ya tetemeko la ardhi wakiwemo wa jimbo lake la Muleba, hatopinga maamuzi hayo kwa kuwa ilikuwa lengo lake kama sheria ingemruhusu kuchukua fedha hizo.
“Katika nchi yetu kuna vikwazo, na nimeweka hili bayana kutokana na jinsi ilivyo, watu wake wanaugonjwa wa kupotosha habari. Na wananchi wakipokea habari huwa hawadadisi na kuchimba kwa undani zaidi kama habari ni ya kweli au uongo, ” amesema.
Hata hivyo, amesema Bungeni kumepelekwa msaada wa sheria ya michango kwa watumishi wa umma ili ionekane kuwa ni ya kijamii na halali na kwamba isiwe inapotoshwa kisiasa.
“Michango mara nyingi imekuwa ikipotoshwa kisiasa, ni kawaida na madhara yake makubwa kwa sababu mtu anapewa joho lisilo mhusu,” amesema.
Profesa Tibaijuka amesema alistahili kuipata tuzo hiyo kutokana na utendaji wake wa kazi mzuri na kwamba ingawa kuna kipindi alichafuliwa kwa kuitwa fisadi, Umoja wa Mataifa ulimfuatilia nyendo zake na kukutwa hana hatia.
“Nimepata tuzo hii kwa niaba ya watanzania kutokana na utendaji kazi wangu, hii tuzo ni ya pili kuipata. Na kwa nilivyochafuliwa wengi walihisi pia hata ubunge nitakosa lakini nimechaguliwa, ” amesema.