SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk
John Magufuli imetenga kiasi cha sh. Bil. 100 katika bajeti ya mwaka 2016/17 kwa
ajili ya ukarabati na upanuzi wa viwanja mbalimbali vya ndege nchini.
Rais Dk. Magufuli alisema hayo juzi katika sherehe
za uzinduzi wa ndege mbili za Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) aina ya
Bombardier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa na serikali, kwenye Kiwanja cha ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambapo viwanja hivyo vitaboreshwa ili
kuwezesha ndege hizo kutua bila wasiwasi.
Mhe. Rais akifafanua zaidi, alisema , kiwanja cha ndege
cha Nduli kilichopo umbali wa kilometa 13 Kaskazini Mashariki mwa Manispaa ya
Iringa, ambacho kipo kwenye kiwango cha lami kitakarabatiwa, ili ndege hizo zitue
na kupaa bila tatizo.
Dk. Magufuli alisema, kiwanja cha Nduli Iringa ni
kiunganishi kikubwa na JNIA na kitatumika kupeleka watalii wanaokwenda
kutembelea mbuga ya wanyama ya Ruaha, wakitokea Mataifa mbalimbali duniani.
Alisema mbali na kiwanja hicho cha Nduli, pia kiwanja
cha Musoma kitawekwa lami, ili nacho kiwe moja ya maeneo ndege hiyo itakwenda,
na kurahisisha usafiri wa watalii watakaokwenda kwenye mbuga ya wanyama ya
Serengeti. Kwa sasa kiwanja cha Musoma kipo katika kiwango cha changarawe na
kinatumika kwa ndege mbalimbali kutua na kupaa.
Kwa mujibu wa Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Nduli,
Bi. Hannah Kibopile, kiwanja hicho kinapokea ndege ndogo zaidi ya saba zenye
uwezo wa kubeba abiria 13, na kati ya hizo tatu zipo kwenye ratiba maalum ya
kila siku na zilizosalia ni za kukodishwa na nyingine zinakwenda mbuga ya
wanyama ya Ruaha.
Bi. Kibopile alisema ndege zinazotua kwenye kiwanja
hicho zinatoka Jijini Dar es Salaam, Sumbawanga, Songea na Mbuga ya Ruaha.
Naye Kaimu Meneja wa Musoma, Bi. Faraja Mayugwa
amesema kiwanja hicho kinapokea ndege zaidi ya nne kwa siku na nyingi zinakuwa
za kukodi zinazopeleka watalii mbugani.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisema “Hii ndege
inaweza kutua katika kiwanja cha aina yeyote; na serikali itaendelea na
ukarabati wa viwanja vya ndege vya pembezoni, ili viwe katika kiwango, ambacho
ndege hizi zitatua na kuruka bila wasiwasi,”.
Akifafanua zaidi Dk. Magufuli alisema serikali
inatarajia kununua ndege nyingine kubwa mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 160
na 242, ambazo zitaanzia safari zake kwenye JNIA kwenda sehemu mbalimbali
duniani kama China au Marekani moja kwa moja, ikiwa ni lengo la kupata abiria hao,
ambao wengi wao watakuwa watalii wanaokuja nchini kutembelea vivutio
mbalimbali. Bombardier inauwezo wa kubeba abiria 76.
Naye Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhe. Prof Makame Mbarawa awali wakati akimkaribisha Mhe. Rais
kuzungumza na wananchi katika ghafla hiyo ya uzinduzi wa ndege, alisema kwa
kuanzia ndege hizo zitatua kwenye viwanja 11 vya ndege, ambavyo ni Kiwanja cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Kilimanjaro (KIA), Zanzibar (AAKIA),
Mwanza, Dodoma, Arusha, Bukoba, Kigoma, Tabora, Mbeya na Mtwara. Pia ndege hiyo itakwenda Comoro.
Mhe. Prof. Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA), kuendelea kufanya upembuzi yakinifu kwa kuangalia
viwanja vingine vya ndege, ambavyo ndege
hizi zitakwenda.
No comments:
Post a Comment