WAFUASI
wawili wa Chadema, akiwemo Mwanamuziki Fulgency Mapunda (32) “Mwana
Cotide”, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na mashitaka ya kumuudhi Rais John Magufuli kupitia mtandao
wa ‘YouTube’.Mapunda na mtayarishaji wa muziki Mnesa Sikabwe (39),
walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Thomas Simba. Wakili wa Serikali, Dereck Mkabatunzi alidai,
Agosti mwaka huu katika eneo la Manzese, washitakiwa hao walisambaza
taarifa zenye lengo la kumuudhi Rais Magufuli.
Inadaiwa kwa makusudi, washitakiwa hao kupitia mtandao wa YouTube,
walisambaza wimbo uliopewa jina la ‘Dikteta Uchwara’ ambao umebeba
maudhui ya kumdhalilisha na kumuudhi Rais Magufuli. Baada ya kusomewa
mashitaka hayo, washitakiwa wote walikana kutenda kosa hilo. Wakili
Mkabatunzi alidai upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea pia hawana
pingamizi na dhamana kwa washitakiwa.
Hakimu Simba alisema,
washitakiwa wataachiwa kwa dhamana endapo watakuwa na wadhamini wawili
wakuaminika watakasaini hati ya dhamana ya Sh milioni 10. Washitakiwa
walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana hadi Oktoba 12, mwaka
huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Imeandikwa na Flora Mwakasala-Habarileo
No comments:
Post a Comment