Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa ya kuuwawa kwa watafiti watatu (3) wakiwa kazini, tukio
lililotokea Oktoba mosi mwaka huu katika kijiji cha Iringa-Mvumi,
Wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma.
Tume
inalaani vikali mauaji haya ya kikatili ya watu wasiokuwa na hatia na
yenye kuitia aibu nchi yetu. Aidha, inaungana na watanzania wengine
nchini kuwapa pole wafiwa na wote walioguswa na msiba huu.
Kwa
mujibu wa taarifa za vyombo vya habari watafiti hao kutoka Chuo cha
Utafiti wa Udongo na Maendeleo ya Ardhi cha Selian, Arusha wakiwa
kijijini hapo kukusanya sampuli za udongo kwa ajili ya utafiti
walivamiwa na kundi la wanakijiji na kushambuliwa kwa mapanga na silaha
za jadi na kisha kuchomwa moto kwa imani kwamba eti walikuwa wanyonya
damu.
Haki
ya kuishi kama zilivyo haki nyingine, inalindwa na sheria na hakuna mtu
anayepaswa kuporwa haki hii ya msingi kiholela. Kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 14, kila mtu anayo haki ya
kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu
wa sheria.
Pia
Mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia
inatoa ulinzi juu ya haki ya mtu kuishi. Baadhi ya Mikataba hiyo ni:
Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la 1948 (Kifungu cha 3) na
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa 1966 (Kifungu cha
6) vinavyoeleza kuwa kila mtu anayo haki ya asili ya kuishi, inayolindwa
kisheria na hakuna atakayenyimwa haki hii ya msingi kiholela.
Hivyo
kuuwawa kwa watafiti hao wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao kwa
taifa ni kitendo kinachopaswa kulaaniwa vikali na kila mwananchi
anayethamini uhai na kuheshimu haki za binadamu.
Kumbukumbu
zinaonyesha kuwa matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi mwao
ni jambo linalojirudiarudia na limekuwa likisababisha uvunjifu wa haki
za binadamu na madhara makubwa kwa jamii, hususan kwa wanawake na
watoto.
Hivyo basi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora:
1. Inaiomba
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kudhibiti mauaji ya
kiholela nchini na kulipatia ufumbuzi tatizo la wananchi kutoheshimu
sheria na kujichukulia sheria mkononi.
2. Inawakumbusha
wananchi kuwa vitendo vya ukatili, mauaji, na matendo yote yanayokiuka
Sheria yanayofanywa na raia wasio wema ni ukiukwaji wa Sheria, haki za
binadamu na misingi ya utawala wa sheira; Hivyo Tume inakemea matendo
haya na kutaka yapigwe vita.
3. Inawataka
wananchi kuheshimu mamlaka zilizopo katika maeneo yao na ngazi
mbalimbali wakitambua kuwa ndio wenye dhamana juu ya masuala mbalimbali
ya kiutendaji katika maeneo husika.
4. Inapendekeza
Kamati za Ulinzi na Usalama katika ngazi za vijiji, vitongoji na kata,
wakiwemo watendaji watimize wajibu wao ili kuepuka madhara kama haya
kujirudia au kutokea katika maeneo mengine.
5. Pia
inapendekeza watendaji wa taasisi za Serikali na binafsi wajitahidi
kuzingatia utaratibu wa kutoa taarifa mapema, ikiwezekana kwa maandishi
kwenye ngazi mbalimbali za uongozi katika maeneo wanayokwenda kufanyia
kazi. Aidha, wazingatie utamaduni wa kujitambulisha kwa viongozi wa
ngazi za chini na kuomba kupatiwa watu wa kuambatana nao katika kazi zao
wawapo katika maeneo hayo.
6. Vilevile
inaona ipo haja ya elimu zaidi kutolewa kwa umma juu ya masuala ya haki
za binadmu na wajibu, sheria, utawala bora na uraia.
7. Inalipongeza
Jeshi la Polisi kwa hatua za kuwakamata watuhumiwa haraka. Aidha,
inaliomba jeshi hilo lifanye uchunguzi wa kina na kuwafikisha mbele ya
vyombo vya sheria wote watakaobainika kuwa walihusika na mauaji na
uharibifu wa mali uliotokea katika tukio hili.
8. Mwisho,
Tume inatoa wito kwa wananchi wa kijiji cha Iringa-Mvumi na maeneo
mengine kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kuhakikisha wote
waliohusika na unyama huu wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo husika
ili sheria ichukue mkondo wake.
Imetolewa na:
(SIGNED)
Mhe. Iddi Ramadhani Mapuri
Makamu Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Oktoba 5, 2016.
No comments:
Post a Comment