Waziri wa Afya,Maendeleo ya
Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameupongeza Umoja wa
waendesha bodaboda Jijini hapa kwa kuchangia mifuko 75 ya sementi kwa
ajili ya ujenzi wa wodi za watoto katika hospitali ya kanda ya Rufaa
ya Mbeya.
Waziri Ummy ametoa pongezi hizo
wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi tatu ambazo
zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mrundikano wa watoto katika
hospitali hiyo
“Kwa niaba ya Serikali
nawashukuru wadau wote waliochangia ujenzi huu ila niseme nimevutiwa
sana na mchango wa Umoja wa waendesha Bodaboda kwa kushiriki ujenzi huu,
mmefanya jambo jema na la Kizalendo katika kutatua changamoto za
utoaji huduma za afya kwa watoto katika hospitali hii ambayo inahudumia
mikoa saba” alisema.
Aidha,Waziri Ummy ametoa rai
kwa makundi mengine ya kijamii hususan wa kanda ya juu kusini kuiga
mfano huo mwema wa bodaboda katika kuchangia kukamilisha ujenzi huo ili
ifikapo Januari,2017 jengo hilo lianze kutumika .
Wakati huohuo Waziri huyo
amewaagiza Waganga wakuu wote wa Mkoa na Wilaya wa hospitali za Umma
nchini kuhakikisha wanatumia vizuri rasilimali zilizopo katika maeneo
yao ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utoaji
huduma za afya kwa wananchi badala ya kusubiri fedha kutoka Serikali
Kuu.
“Serikali imedhamiria kuboresha
huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa kanda za juu kusini
tumejipanga kuhakikisha kuwa ujenzi wa jengo la uchunguzi (Diognistic
Centre) lililokwama kwa takribani miaka saba unakamilika ndani ya
mwaka mmoja”,hii itawaondolea kero wananchi wa nyanda hii kwenda Dar es
Salaam kwa ajili ya huduma za vipimo vya kiuchunguzi wa magonjwa kama
TC Scan
Kuhusu matibabu ya saratani kwa
njia ya dawa (Chemotherapy Waziri Ummy alisema matibabu hayo yataanza
kutolewa mapema mwakani na hivyo itapunguza kero kwa wananchi wa kanda
ya Mbeya kwenda katika hospitali ya saratani ya Ocean Road.
Awali, akitoa taarifa ya ujenzi
huo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya, Dkt.
Godlove Mbwanji alisema ujenzi wa wodi hizo ambao utagharimu shilingi
milioni 300 ambazo zinatokana na fedha za ndani za hospitali hiyo pamoja
na michango ya wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Mbeya.Jengo hilo litakuwa
na vitanda 76 na hivyo kumaliza kabisa tatizo la wagonjwa kulala chini.
Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya inahudumia mikoa ya
Iringa,Njombe,Songwe,Katavi, Ruvuma,Rukwa Iringa pamoja na Mbeya
No comments:
Post a Comment