Siku
moja baada ya Mkoa wa Mtwara kutangazwa kushika mkia katika matokeo ya
upimaji wa kitaifa wa wanafunzi wa kidato cha pili, Mkuu wa Mkoa huo,
Halima Dendego amesema hayajatokea kwa bahati mbaya.
Mkuu
huyo alisema licha ya kutofurahishwa na matokeo hayo, alitarajia hali
ingekuwa hivyo kutokana na suala la elimu kutopewa kipaumbele mkoani
Mtwara.
Alisema
tangu ateuliwe kuongoza mkoa huo, amegundua kuwa mambo mengi hayaendi
sawa katika elimu, hali iliyomlazimu kujiwekea mikakati ya kujipanga
upya.
“Nimekuja
Mtwara nimegundua mambo hayako sawa, nikajaribu kutafuta kiini, ndiyo
nikabaini hakuna mwamko wa elimu, walimu siyo wabunifu.
"Wanashindwa kuangalia mazingira yaliyopo na kufundisha kulingana nayo. Utoro pia umekithiri,” alisema.
Aliitaja
changamoto nyingine aliyoigundua kuwa ni udanganyifu kwenye mitihani
hasa ya kuhitimu elimu ya msingi ambayo watoto wengi hufaulu kwenda
sekondari.
“Hao
watoto waliofanya mtihani wa kidato cha pili mwaka jana walifaulu
vizuri mtihani wa darasa la saba iweje leo washindwe, hapo ndipo
utagundua kuna mazingira ya udanganyifu.
“Watoto
wengi wameingia sekondari kwa udanganyifu kwa hiyo matokeo haya
tuliyajua, jambo hili nimedhamiria kulikomesha lengo langu ni kuuweka
mkoa wetu katika hali nzuri,” alisema Dendego
Alisema
Januari 14, aliitisha mkutano wa wadau wa elimu; viongozi wa dini, wa
halmashauri na mitaa kujadiliana namna ya kuinua kiwango cha elimu
mkoani humo.
“Tumeshapeana majukumu kila mtu katika eneo lake kuhamasisha kuhusu umuhimu wa elimu, hasa viongozi wa dini kwa waumini wao.
“Walimu
nao wanatakiwa kufundisha kulingana na mazingira. Ubunifu ukiongezeka
katika ufundishaji, taratibu tunaweza kubadilisha upepo. Naamini
tukishirikiana suala hili litafanikiwa,” alisema.
Ofisa Elimu wa mkoa huo, Fatuma Kilimia alisema amedhamiria kuimarisha usimamizi ili kumaliza tatizo la udanganyifu.
“Tatizo
hili linaonekana lilikuwapo. Hawa watoto walioanguka mtihani huu mwaka
2014 walishika nafasi ya nane kitaifa kwenye mtihani wa darasa la saba.
Matokeo ni mabaya na hakuna namna ya kufanya zaidi ya kuimarisha
usimamizi na ufuatiliaji kwa walimu. Watoto hawawezi kufanya vizuri bila
kufundishwa,” alisema.
Katika orodha ya shule zenye matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015, Mkoa wa Mtwara uliingiza shule 33.
Shule hizo zilikuwa kwenye mstari mwekundu ikimaanisha kuwa wanafunzi wake walifanya vibaya kupita kiasi kwenye mtihani huo.
Chingungwe,
Naputa, Msimbati na Salama ni miongoni mwa shule za sekondari
zilizokuwa kwenye mstari mwekundu katika matokeo ya kidato cha nne mwaka
jana, Msimbati ikishika namba sita na Naputa namba 10.
Akizungumzia
matokeo hayo, Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch
alisema mazingira magumu ya kazi mkoani Mtwara yamechangia kwa kiasi
kikubwa matokeo hayo.
Alisema
shule nyingi zimekosa walimu kutokana na mazingira magumu na Serikali
imeshindwa kulifanyia kazi suala hilo ili kupata ufumbuzi.
“Tukubali
kuwa Mtwara ni eneo lenye mazingira magumu ya kazi. Shule hazina walimu
na kwa bahati mbaya Serikali imekataa kutekeleza pendekezo la CWT la
kutoa posho kwa walimu walio katika mazingira magumu,” alisema.
Oluoch
alisema changamoto nyingine inayodumaza kiwango cha elimu Mtwara ni
kukithiri kwa mila na desturi, hivyo kuwazuia watoto kupata haki ya
elimu.
No comments:
Post a Comment