Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia Wambura (katikati) akichangia wakati wa majadiliano leo Jijini Dar es Salaam na wadau wa Sekta ya Utamaduni katika kukuza na kukifanya kiswahili kuwa bidhaa yenye thamani. Kushoto ni Waziri wa Habari Mhe. Nape Moses Nnauye na kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao |
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na wadau wa Sekta ya Utamaduni (hawapo pichani) walipokutana leo Jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa yenye thamani ndani na nje ya nchi. |
: Baadhi ya Wadau wa Sekta ya Utamaduni wakifuatilia kwa makini hoja zilizokua zikiendelea wakati wa majadiliano na viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kujadili namna ya kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa yenye thamani ndani na nje ya nchi leo Jijini Dar es Salaam |
Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Dkt. Selemani Sewangi akitoa taarifa ya namna Kiswahili kinavoendelea kukua wakati wa majadiliano na wadau wa sekta ya Utamaduni kujadili namna ya kukuza na kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa yenye thamani ndani na nje ya nchi leo Jijini Dar es Salaam. |
Mdau wa Utamaduni Mama Mipango akichangia mada wakati wa majadiliano na wadau wa sekta ya Utamaduni kujadili namna ya kukuza na kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa yenye thamani ndani na nje ya nchi leo Jijini Dar es Salaam. |
: Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (waliokaa katikati) katika picha
ya pamoja na wadau wa sekta ya Utamaduni walipokutana kujadili namna ya
kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa yenye thamani leo Jijini Dar es Salaam.
Wapili kulia waliokaa ni Naibu Waziri wa Habari Mhe. Annastazia
Wambura, Wapili kushoto waliokaa ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari Prof.
Elisante Ole Gabriel, na wakwanza kushoto waliokaa ni Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Habari Bibi. Nuru Millao.
Picha na: Genofeva Matemu – WHUSM
………………………………………………………………………………….
Na: Genofeva Matemu – WHUSM
Tarehe: 14/02/2017
Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo imeanza kutekeleza malengo iliyojiwekea ya kuifanya
Lugha ya Kiswahili kuwa bidhaa yenye thamani ili iweze kupata soko na
kutumika duniani kote katika kurahisisha mawasiliano ya watumiaji wa
lugha hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Waziri
mwenye dhamana ya Sekta na Utamaduni Mhe. Nape Moses Nnauye alipokua
akizungumza na wadau wa Sekta hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
“Tumejipanga kuangalia changamoto
zinazotokana na Sera na Sheria tulizonazo, changamoto za kirasilimali
na mambo ya kiutashi kwani kwa kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo
Kiswahili kitaendelea kuwa bidhaa ambayo itavuka mipaka ya nchi na
kuitangaza nchi yetu” amesema Mhe. Nnauye.
Akizungumza wakati wa Mkutano huo
Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Dkt. Selemani
Sewangi amewataka waandishi wa vitabu vya Kiswahili kuzingatia weledi wa
matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili wakati wa uandishi wa vitabu ili
kuweza kuisaidia jamii hasa mashuleni kujua misamiati fasaha ya lugha
hiyo.
Kwa upande wake mdau wa Utamaduni
nchini Dkt. Musa Hans ameiomba serikali kuhamasisha wageni wote
wanaoingia nchini kujifunza lugha ya Kiswahili na kuandaa mwongozo kwa
kushirikiana na Wizara ya Elimu utakaowataka watoto wote wanaoingia
sekondari kuwa na kamusi za Kiswahili na kamusi za Kiswahili Kingereza
zitakazowasaidia kujua misamihati ya lugha ya Kiswahili.
Naye Mdau wa Utamaduni mama
Mipango ameipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais
Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kutafuta njia mbalimbali za
kueneza na kukuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.
Katika kuendeleza ukuaji wa Lugha
ya Kiswahili Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli amekua mstari wa mbele kutumia lugha ya Kiswahili katika
shughuli mbalimbali za kiserikali kama vile Mkutano wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki na Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) ambapo kwa kufanya
hivyo lugha hii imeweza kusambaa kwa kasi zaidi.
|
No comments:
Post a Comment