Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Mtu yeyote atakaye ruhusu mtoto
chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la mchezo
wa kubahatisha (kamari) anahesabiwa kufanya kosa.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Dkt. Ashatu Kijaji ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa
akijibu swali la Mbunge Viti Maalum Asha Abdullah Juma juu ya kuongezeka
kwa maduka ya kucheza Kamari yanayojulikana kama Jack Pot katika miji
mingi hapa nchini hivyo kusababisha uvunjifu wa maadili na nguvu kazi ya
vijana.
“Michezo yote ya kubahatisha
ikiwemo kamari (slots machines) inaendeshwa kwa mujibu wa sheria ya Bodi
ya Michezo ya kubahatisha namba 4 ya mwaka 2003, sura 41 pamoja na
Kanuni zake,” alifafanua Dkt. Kijaji.
Aliendelea kwa kusema kuwa, kwa
mujibu wa sheria hiyo hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kuendesha
biashara ya michezo ya kubahatisha bila kuwa na leseni kutoka Bodi ya
Michezo ya kubahatisha pamoja na vibali vingine vinavyotolewa na mamlaka
nyingine za biashara.
Vile vile sheria hiyo inakataza
watoto wenye umri chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia, kukaa au
kuzururazurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha.
Aidha mtu yoyote ambaye atamruhusu
mtoto chini ya miaka 18, kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la
mchezo wa kubahatisha anahesabika kufanya kosa na anastahili kulipa
faini ya shilingi 500,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote
kwa pamoja.
Dkt. Kijaji amesema kuwa ikiwa kosa hilo litafanywa na mwendesha mchezo wa kubahatisha, Bodi inamamlaka ya kumfutia leseni.
Hivyo basi, wajibu wa Serikali ni kuzuia watoto na vijana walio chini ya miaka 18 kucheza michezo ya kubahatisha.
Pia, Dkt. Kijaji ametoa rai kwa
wazazi na walezi kuwazuia vijana wao kucheza michezo ya kubahatisha pale
wanapoona kuwa uchezaji wao unakuwa na matokeo hasi.
Hata hivyo amesema kuwa, michezo
hiyo inaendeshwa kwa mujibu na sheria kama shughuli nyingine. Jambo la
msingi ni kuhakikisha kuwa, wanaoendesha michezo hiyo wanazingatia
sheria na kanuni zilizowekwa pamoja na wazazi, walezi na jamii
kuhakikisha vijana wanazingatiia mila na desturi zinazolinda maadili ya
Kitanzania wanapokuwa wanajishughulisha na shughuli halali za kiuchumi.
|
February 8, 2017
MZAZI ATAKAYEMRUHUSU MTOTO WAKE KUSHIRIKI KAMARI KUSHTAKIWA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment