Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani (kulia) akisalimiana na Meneja
Mkuu wa Redio AFM ya Dodoma Bw. Tatenda J. Nyawo baada ya kutoa elimu ya
mpiga kura kupitia redio hiyo hivi karibuni.
………………………………………………………………………..
Hussein Makame, NEC-aliyekuwa Dodoma
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imesema kuwa kura zilizoharibika zinazopatikana kwenye chaguzi
zinasababishwa na wapiga kura wengi kukosa elimu ya mpiga kura.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Tume hiyo Bw. Kailima Ramadhani wakati akijibu swali la
mmoja wa watangazaji wa kituo cha Redio AFM cha mkoani Dodoma katika
mfululizo wa kutoa elimu ya mpiga kura kupitia vituo vya redio.
Mtangazaji huyo alihoji kwa nini
inajitokeza unapotokea uchaguzi kunakuwa na kura zisizo halili au kura
zilizoharibika wakati Tume imekuwa ikitoa elimu ya mpiga kura katika
chaguzi zilizopita.
Bw. Kailima alijibu kuwa
kinachosababisha hali hiyo ni ukosefu wa elimu ya mpiga kura kwa
wananchi, na ndio maana Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi iliona umuhimu wa kutoa elimu hiyo katika
kipindi chote cha mwaka.
“Mkurugenzi tusalie hapo kwenye
kura halali na zilizoharibika, elimu hii umekuwa ukiitoa maeneo
mbalimbali na leo tuko hapa AFM, kwa nini hadi leo tunakuwa na kura
zilizoharibika na kura zisizo halali” alihoji.
Akijibu swali hilo, Bw. Kailima
alisema ukosefu wa elimu ya mpiga kura ndio unaosababisha hali hiyo na
ndio maana Katiba iliona kuna umuhimu wa Tume kutoa elimu hiyo kwa muda
wote bada ya kutoa wakati wa kipindi cha uchaguzi.
“Ukiendea kifungu cha 4C cha
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kimesema Tume itatoa elimu ya mpiga
kura.Lakini tumekuwa na tatizo la kutotoa elimu ya mpiga kura baada ya
uchaguzi na imekuwa ikitolewa wakati wa uchaguzi baada ya uteuzi na
wagombea wakiteuliwa leo kesho kampeni inaanza” alisema Bw. Kailima na
kuongeza:
“Kama Tume na wadau wanaanza
kutoa elimu ya mpiga kura katika kipindi hicho, sasa mpiga kura
atazingatia kusikiliza kampeni za chama badala ya kusikiliza utaratibu
mzima wa namna ya kupiga kura kama”
Alisema kwa kuwa Tume imeanza
kutoa elimu ya mpiga kura katika kipindi chote cha mwaka itasaidia sana
ifikapo uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kura zilizoharibika zitakuwa chache
sana.
Kuhusu kura kuharibika, Bw.
Kailima alisema kura yoyote iliyowekwa alama ya vema kwenye eneo la
mgombea itahesabika kuwa kura halali.
“Kwa mujibu wa muongozo na
maelekezo yaliyotolewa na Tume kwa wasiamamizi wa uchaguzi, alama yoyote
ikiwemo ya X itakayowekwa kwenye chumba cha picha ya mgombea au jina la
chama cha mgombea au kwenye chumba cha wazi itakubalika kwamba ni alama
halali” alisema.
Alifafanua kuwa karatasi ya kura
itakataliwa iwapo haina muhuri wa kituo au itakuwa na kitu au alama
inayomtambulisha mpiga kura na iwapo, haijawekwa alama inayotambuliwa
kuwa ni halali.
Aliongeza kuwa karatasi ya kura
itakayopigwa kwa mgombea aliyejitoa kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi au
ikawekwa alama kwa mgombea zaidi ya mmoja na iwapo haina alama yoyote,
itakataliwa.
Hata hivyo, Bw. Kailima aliongeza
kuwa uamuzi wa uhalali wa kura kituoni utaamuliwa na msimamizi wa kituo
iwapo atarijiridhisha kuwa kura imeharibika na haiwezi kuhesabiwa na
ataikataa na haitahesabiwa.
Tume imeanza kutekeleza mpango wa
kutoa elimu ya mpiga kura kupitia vituo vya redio za kijamii katika
mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ikiwa ni sehemu ya
kutekeleza matakwa ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya kutoa elimu ya
mpiga kura muda wote.
No comments:
Post a Comment