Warsha ya wachora vibonzo vijana.
Tarehe 7-9/6/2017, NMF
itaendesha warsha ya siku tatu itakayofanyika katika ukumbi wa Nafasi
Art Space, Dar es Salaam inakusudia kuwajengea uwezo wachora vibonzo
vijana ambao tayari wanafanya kazi kwenye vyombo vya habari na wale
ambao bado hawajapata nafasi hiyo.
Kutokana na mabadiliko ya
teknolojia duniani, NMF inaamini kuwa kuna umuhimu wa wachora vibonzo
wakapata mafunzo ya mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko hayo.
Warsha hiyo itafuatiwa na
onesho la wazi la vibonzo vilivyochorwa katika warsha hiyo siku ya
Jumamosi, tarehe 10/6/2017 kuanzia saa 10.00 alasiri mpaka 12 jioni
katika katika ukumbi huo huo ambapo wakaazi mbalimbali wanakaribishwa.
Hakutakuwa na kiingilio.
NMF inayoamini kuwa kipaji
kinakuwa na maana pale tu kinapoibuliwa, endelezwa, nufaisha msanii na
Taifa, inatoa shukrani kwa Ubalozi wa Uswis nchini Tanzania, Nafasi Art
Space na RUKA Kipro kwa kuwezesha warsha hii kufanyika.
NMF inatoa wito kwa wadau
mbalimbali kuiunga mkono hasa katika eneo la kuwajengea uwezo vijana
wenye ndoto ya kuja kuwa wasanii hodari nchini.
Kifo cha Mzee Fransis Kanyasu Maige.
NMF inatoa pole kwa ndugu,
familia na jamaa wa mchoraji mkongwe, Mzee Fransis Kanyasu Maige
aliyefariki hivi karibu jijini Dar es Salaam.
NMF imesikitishwa na hali ya
maisha aliyokuwa akiishi mkongwe huyo na kwamba hicho ni kiashiria tosha
kuwa kuna changamoto nyingi kwenye mfumo wa sanaa nchini na kwamba
umefika wakati sasa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikatoa
ulinzi kwenye ubunifu kwa kutambua aina ya tatu ya mali yaani “Mali
Isiyoshikika,” kwani wasanii wamekuwa wakitumika kuhamasisha maendeleo
lakini kwa bahati mbaya wengi wao sanaa huwa haiwanufaishi!
Aidha, NMF inafahamu kuwa
Serikali kwa kushirikiana na mashirikisho ya sanaa nchini ipo kwenye
hatua ya awali ya ukusanyaji maoni kwa ajili ya “sera mpya ya sanaa”
ambayo NMF inaamini itakuja na majibu yatakayotatua changamoto
zinazowakabili wasanii na mfumo mzima wa sanaa.
NMF inaunga mkono hatua hiyo na
inaiomba Serikali kuongeza nguvu hasa eneo la rasilimali fedha ili
kuwezesha ukusanyaji wa maoni ikiwezekana nchi nzima.
Nathan Mpangala Foundation
(NMF), No.5286, yenye makao yake jijini Dar es Salaam, ni asasi
isiyokuwa ya kiserikali iliyosajiliwa mwishoni mwa mwaka jana kwa Wakala
wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ikiwa na malengo kadhaa ikiwemo
mafunzo ya sanaa.
Imetolewa na;
Nathan Mpangala,
NMF, Mwenyekiti
*******************************
Yours faithfully,
Nathan Mpangala,
Chairperson
NMF, Board of Trustees
No comments:
Post a Comment