Naomba nianze kwa kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana mahali hapa siku ya leo tukiwa wazima wa Afya,
Lakini
pia nichukuwe nafasi hii kuishukuru Serikali ya awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dr.Joseph
Pombe Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ninaoupata katika uendeshaji wa
mpira wa miguu, nimekuwa karibu sana na Serikali kuhakikisha juhudi zetu
za kuendeleza mpira zinafanikiwa kwa kasi kubwa sana na mafanikio ya
ujio wa Rais wa FIFA ni kielelezo cha karibuni kuonyesha ushirikiano
mkubwa tunaoupata toka kwa Serikali hasa Waziri mwenye dhamana ya
michezo Mh.Dr,Harrison Mwakyembe na timu yake.
Lakini
niwashukuru kwa nafasi ya kipekee ndugu zangu Waandishi wa Habari kwa
kazi kubwa mnayoifanya kuhabarisha umma kuhusu habari za mpira wa
miguu,Pia pongezi zenu kwa kazi nzuri mliyoifanya wakati wa ujio wa
FIFA, mlifanya kazi kubwa sana kutangaza ziara ya Rais wa FIFA, mmetupa
heshima kubwa sana.
Ndugu
zangu, leo nitaongelea mambo makubwa mawili ili waTanzania wapate
kufahamu kinachoendelea katika mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini.
Moja
nitaongelea kuhusu mambo ambayo tumeyafanya kwa kipindi cha miezi saba
nilichokuwepo madarakani lakini la pili ni mambo yanayoendelea sasa hivi
kwenye Shirikisho.
MAMBO AMBAYO TUMEYAFANYA KWA MIEZI SABA TOKA TUINGIE MADARAKANI
HALI NA SHUGHULI ZA TAASISI
Kwa
Mazingatio ya Utekelezaji Makini na wa Maendeleo wa Shughuli za Taasisi
Tulitambulisha Muelekeo na Dira ya TFF ambapo Kazi iliyo Mbele yetu ni
Kuzitoa na Kuimarisha Utambuzi na Utekelezaji wake. Sasa ni wakati
Tunajiandaa Kutoa baadhi ya Mipango yetu na kutoa Dira za Utekelezaji
wake. Pamoja na Mipango hiyo Bado TFF tumekuwa Tukitekeleza Shughuli za
Mpira katika Mgawanyiko wake na labda kwa kifupi kugusia Miongoni mwake.
Mashindano.
Tumeendesha
mashindano mbalimbali kwa ufanisi mkubwa yakiwemo mashindano ya Azam
Sports Federation Cup, Ligi ndogo ya Wanawake kwa ajili ya kupata timu
za kupanda daraja,Ligi Kuu ya Wanawake hatua ya makundi na hatua ya nane
bora inayoendelea,Mashindano ya soka la ufukweni kwa timu za vyuo
vikuu,Mashindano ya kimataifa ya soka la ufukweni yajulikanayo COPA DAR
ES SALAAM.
Azam Sports Federation cup;
Mashindano
hayo kwa msimu huu 2017/18 tumeyaendesha kwa ufanisi na umakini mkubwa
tofauti na huko nyuma kwa kuhakikisha upangaji wa ratiba umekuwa wa wazi
usio na upendeleo wowote ule hivyo kupunguza malalamiko,jambo lingine
tulihakikisha timu zote zinapata stahiki zao kwa wakati na kiwango
kilichopangwa,kadiri tunavyoelekea hatua za mwisho wa mashindano
tutahakikisha changamoto zote zilizojitokeza huko nyuma tunakabiliana
nazo na kuzitatua ili kuhakikisha mashindano hayo yanaisha vizuri.
Ligi kuu ya Wanawake;
Mwaka
huu tulianza kucheza Ligi ndogo ya Wanawake kutafuta timu za kupanda
Ligi Kuu ya Wanawake katika vituo vya Dar es salaam na Dodoma,ikafuatiwa
na Ligi ya Wanawake katika kituo cha Arusha na Dar es Salaam ili kupata
Timu 8 za kucheza hatua ya Nane bora ya Ligi hiyo.
Katika
hatua ya makundi, TFF ilizigharamia timu zote kwa asilimia 100 kuanzia
malazi, usafiri, chakula, gharama za maadalizi ya timu na nauli ya
kwenda na kurudi,ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya mpira wa
miguu wa Wanawake kwa TFF kugharamia kwa kiwango hiki.
Katika
hatua ya Nane bora ya Serengeti Lite Women Premier League vilabu vyote
vilishapewa fedha zao kwa ajili ya hatua ya kwanza ambayo imesimama
kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ya Wanawake(Twiga Stars) ambayo
inajiandaa na mashindano ya kufuzu michuano ya Afrika kwa Wanawake
ambapo tayari timu ya Taifa ipo kambini ikijiandaa na mchezo huo dhidi
ya Zambia.
Taasisi
iliendesha kwa mafanikio makubwa mashindano ya soka la ufukweni (Copa
Dar es Salaam) kwa kuzialika timu za Uganda, Malawi, Zanzibar na wenyeji
Tanzania bara ambazo tulizigharamia malazi, chakula na usafiri wa
ndani.
PROGRAMU ZA TIMU ZA TAIFA
Toka tumeingia madarakani, tumekuwa tunafanyia kazi program mbalimbali za maendeleo ya Timu za Taifa.
Taifa Stars
Tumekuwa tukiendelea na program mbalimbali za Timu ya Taifa za kuhakikisha inafuzu Fainali za kombe la mataifa Afrika 2019.
Kuhakikisha
hili Taifa Stars ilicheza na Benin, Malawi, Botswana na wiki hii
tunacheza na Algeria pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
katika kalenda ya mechi za kimataifa ya FIFA.
Ili kuongeza hamasa ya wachezaji tumeongeza posho ya ndani kwa asilimia 100 na asilimia 50 kwa posho za nje.
Kilimanjaro Stars
Timu
yetu ya Tanzania bara ilishiriki mashindano ya CECAFA yaliyofanyika
nchini Kenya mwezi Desemba 2017, mbali na kushiriki ili ichukuwe kombe
sababu nyingine ilikuwa ni kuendelea kupata mechi nyingi za kimataifa.
Timu
ilicheza dhidi ya Rwanda, Kenya, Zanzibar na Libya, Tunaamini kwa
wachezaji vijana waliokuwa sehemu ya kikosi hicho imewajengea uwezo
katika soka la kimataifa.
Timu za Taifa za Vijana
Katika
eneo hili tumekuwa na mpango wa muda mrefu kuhakikisha vijana wa timu
zetu za Taifa za miaka chini ya 23, 20, 17 na 13 zinakuwa na maandalizi
bora na kwa kuanzia toka tuingie madarakani tumekuwa na kambi za timu za
vijana kila mwezi kwa kuwakutanisha siku 14 za mazoezi na kuwatafutia
mechi za kirafiki za kimataifa.
Timu ya U23
Timu
ya Taifa chini ya miaka 23 ambayo ni kikosi cha pili cha timu ya Taifa
kimeshaitwa kambini mara kadhaa na tumethibitisha kushiriki mashindano
ya Olimpiki ambayo fainali zake zitafanyika nchini Japan, lengo ikiwa
ni kuhakikisha tunawapatia vijana hawa mechi nyingi za kimataifa ili
wawe tayari.
Timu ya Vijana U20
Timu
ya Vijana U20 ambapo jana ilicheza na Morocco na Jumatano itacheza na
Msumbiji, ikiwa ni maandalizi ya mechi dhidi ya timu ya vijana chini ya
miaka 20 ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo(DRC) ikiwa ni
mchezo wa kufuzu fainali za Vijana Afrika chini ya miaka 20.
Timu ya Vijana U16
Timu
hii nayo imekuwa ikiingia kambini kila mwezi na hata sasa hivi
ninavyozungumza na nyinyi, timu hii ipo kambini ikijiandaa kwa
mashindano ya CECAFA na tunafanya jitihada za kuhakikisha inapata mechi
mbili za kirafiki za kimataifa kabla haijaenda Burundi.
Timu hii ndiyo ambayo itashiriki fainali za Afrika chini ya miaka 17 zitakazofanyika hapa nchini mwaka 2019.
Baada
ya kutoka Burundi itakuwa na program maalum kwa ajili ya kujiandaa kwa
mashindano mengine ya kufuzu AFCON U17, 2019 ambayo yatafanyika nchini
mwezi Agosti ambayo lengo ni kupata mwakilishi wa CECAFA na vijana wetu
watashiriki kama wenyeji. TFF imeamua kushirikisha Timu yenye Umri mdogo
zaidi kwa u17 bila ya kujali Matokeo zaidi ya Ujenzi wa timu kwa
kuandaa timu moja katika matukio yote haya ili kuiweka tayari kwa
Mashindano ya u17 ya 2019 mwakani ambapo vijana hawa ndio watakuwa rasmi
u17
Timu ya Vijana ya U13
Timu
ya Vijana ya U13 katika kutafuta namna ya Kuwaimarisha vijana hawa
baada ya Utambuzi na Uteuzi wa timu imepata nafasi ya kushiriki
mashindano ya kirafiki ya vijana chini ya miaka 13 yatakayofanyika
nchini Ubelgiji mwezi Agosti 2018,Tayari orodha ya kwanza ya wachezaji
69 waliopatikana katika mashindano ya shule za msingi (UMITASHUMITA)
ipo TFF na idara ya ufundi inaandaa utaratibu wa kuwaita pamoja na
kupata michezo ya kirafiki dhidi ya Zanzibar kwa ajili ya kupata kikosi
cha pamoja cha Tanzania.
Timu ya Taifa ya Wanawake U20
Tumeanza
kuandaa kikosi cha Vijana cha timu ya taifa ya Wanawake U20 ili kuwa na
kikosi bora cha Twiga Stars kilichoandaliwa kwa muda mrefu na tayari
ilishacheza michuano ya kufuzu fainali za vijana za Afrika chini ya
miaka 20 na kutolewa na Nigeria.
Baadhi
ya wachezaji wa timu hii wamepandishwa kikosi cha wakubwa na sehemu
kubwa wanacheza Ligi Kuu ya Wanawake kupitia vilabu mbalimbali.
Tutaendelea na utaratibu wa kuwaita kambini kila wakati kutakapokuwa na nafasi ili kuzidi kuimarisha kikosi.
Twiga Stars
Kikosi
cha Twiga Stars kimeingia kambini kwaajili ya maandalizi ya mashindano
ya kufuzu fainali za Africa kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Ghana
baadaye mwaka huu.
Twiga
Stars inakabiliwa na mchezo dhidi ya Timu ya Taifa ya Zambia
utakaochezwa Aprili 4,2018 Uwanja wa Taifa na marudiano kuwa Aprili
8,2018 nchini Zambia.
MAPATO NA MATUMIZI
MAPATO
Katika
kipindi cha miezi Saba(7),Shirikisho limefanikiwa kukusanya kiasi cha
Tzs 3,670,397,199.00 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali ambavyo ni
pamoja na mapato kutoka kwa wadhamini Tzs 2,295,472,151 sawa na 62.5%ya
mapato yote, makusanyo ya viingilio uwanjani Tzs 378,139,866 sawa
na10.3%. 27.2% ilitokana na Fedha kutoka CAF na FIFA.
MATUMIZI
Katika
kipindi hiki Shirikisho lilitumia kiasi cha Tzs 3,752,001,171.00.
Sehemu kubwa ya matumizi yalielekezwa kwenye usimamizi wa ligi
mbalimbali pamoja na kuandaa timu za taifa ambapo jumla ya Tzs
2,409,150,732 sawa na 64% ya matumizi yote zilitumika.
Asilimia
36 ya Fedha zilizobaki ilitumika kulipia madeni ya Taasisi, Kulipa
mishahara ya wafanyakazi, kusaidia mikoa katika maeneo ya miundo mbinu,
kuwajengea uwezo wafanyakazi pamoja na kuendesha mafunzo mbalimbali.
Kama
Rais wa TFF sijapokea HOJA wala USHAURI wala MAPENDEKEZO yoyote kutoka
kwa Wajumbe wangu katika Ngazi zote kuhusiana na Matumizi ya Taasisi,
Nasikitika kama kuna anayedai amehoji sijui wapi kwa kuwa kama Rais
sijapokea hoja yoyote wala kuwasilishwa katika kikao cha Kamati ya
Utendaji iliyopita ambayo Taarifa ya Kamati ya Fedha iliwasilishwa
nakupokelewa na kupitishwa na Kamati ya Utendaji.
MADENI
Katika
kipindi hiki,Shirikisho lilianza zoezi la kutathmini madeni
iliyoyarithi kutoka kwenye Uongozi uliopita, ambapo deni hilo linafikia
Tzs 2,172,000,000linalodaiwa na watoa huduma mbalimbali,
wafanyakazi,wachezaji na makocha.
Asilimia
kubwa ya deni hili lilitokana na malimbikizo ya deni la TRA, Workers
Compensation Fund na NSSF ambalo lililimbikizwa kwa zaidi ya miaka
miwili.
Shirikisho
lilifanikiwa kulipa deni lote la michango ya wafanyakazi NSSF jumla ya
Tzs 88,000,000 zilizokuwa hazijalipwa kipindi cha miaka miwili, na
lilifanya majadiliano na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu ulipaji deni
la kodi linalofikia Tzs 1,077,000,000, ambapo jumla ya Tzs 315,000,000
zimelipwa nakiasi kilichobaki tumekubaliana kitalipwa kwa awamu kadhaa
mpaka deni lote litakapomalizika.
Pia
shirikisho limefanikiwa kupunguza mishahara kwa wafanyakazi kutoka Tzs
85,063,092.00 mpaka kufikia 50,000,000.00 baada ya kupunguza idadi ya
wafanyakazi kutoka 44 mpaka 21.
Baada
ya kuingia madarakani tulifanya majadiliano na makocha wa timu za Taifa
kuhusu uhalisia wa malipo yao na kufanikiwa kuokoa zaidi ya dola laki
mbili(USD 200,000) kwenye mikataba yao na fedha zilizookolewa zitasaidia
shughuli nyingine za mpira wa miguu.
UFUNDI
1. Kliniki iliyoendeshwa na Kocha PiaSundhage kutoka Sweden
2. Kozi ya ngazi ya awali ya makocha wa mpira wa miguu
ilifanyika katika mikoa ya Kigoma,Songwe, Lindi, Morogoro na Pwani
3. Kozi ya ngazi ya kati ya makocha wa mpira wa miguu
Ilifanyika katika mikoa ya Kigoma mara mbili, Manyara na Morogoro.
4.Grassroot & Live your goal project
Kozi hii ilifanyika katika mikoa ya Lindi ambapo washiriki walitoka katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Pia
kozi nyingine ilifanyika katika mkoa wa Mbeya ambapo washiriki walikuwa
ni kutoka katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Katavi, Songwe na Rukwa
Aidha hii kozi ilifanyika Kigoma na kushirikisha washiriki wa mikoa ya Kigoma na Tabora.
5.Mafunzo ya awali ya Utawala mikoani
Kuna kozi ya utawala na masoko iliyofanyika Dar es Salaam ili kuwaongezea watu wa masoko uwezo wa kuwavutia wadhamini.
6.Mafunzo ya waamuzi
Mafunzo ya waamuzi wa FIFA na Waamuzi wa ngazi ya juu yalifanyika mara tatu jijini Dar es Salaam.
7. Kozi ya kupandisha daraja kwa Waamuzi
Kozi hii ilifanyika mara mbili katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.
8. Ziara za Mafunzo na kubadilishana uzoefu
Zilifanyika ziara mbalimbali za Waamuzi wetu za kubadilishana uzoefu katika nchi mbalimbali.
9. Mpango wa ugawaji wa vifaa vya vijana na mafunzo
Tulipoingia
madarakani tulikuta uongozi uliopita wameshanunua mipira na imekaa
stoo, katika kutekeleza azma ya maendeleo ya vijana ili tuwe na timu za
Taifa imara Shirikisho limegawa mipira (100 kwa kila Mkoa) saizi 4 na 3
kwa Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, Mikoa imepewa vifaa vya
kufundishia (cones and markers) ili vijana wapate fursa ya kuonesha na
kuendeleza vipaji vyao kwa maslahi ya Mpira hapa nchini.
Uzinduzi wa zoezi hili ambalo linategemewa kuwa endelevu lilifanyika Uwanja wa Taifa Agosti 3, 2017.
Rais
wa TFF aliwakabidhi wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa niaba ya Mikoa
yao kwenye Kanda husika, Kwa upande wa Zanzibar Katibu Mkuu wa ZFA
alikabidhiwa mipira hiyo kwa ajili ya Mikoa ya Zanzibar.
MASOKO NA HABARI
Tumeendelea
kuongeza wadhamini katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha Taasisi
inanufaika na bidhaa zake.Lakini pia tumeendelea kuimarisha idara ya
habari kwa kuwanunulia nyezo za kufanyia kazi.
UTAWALA BORA
Katika
kipindi hiki cha Miezi saba nimesimamia eneo hili kwa uadilifu mkubwa,
Kamati zimekuwa zinakutana kabla ya vikao vya Kamati ya Utendaji ili
kuhakikisha kila mmoja anashirikishwa.
Mfano,
Wakati nilipokuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha,kwa miaka 4 nilikaa
kikao kimoja cha Kamati ya Fedha,Katika Utawala wangu aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ndani ya miezi saba ameitisha vikao
visivyopungua vitano.
Nilimuagiza
Kaimu Katibu Mkuu kuhakikisha kila Kamati ya Fedha inapohitaji kukutana
ahakikishe inakutana na Mtendaji Mkuu amekuwa anatekeleza.
Na
kwa sababu nafasi ya Makamu wa Raisi Kikatiba ndiye Mwenyekiti wa
Kamati ya Fedha na Mipango, basi hata mazungumzo ya Mkataba wa Udhamini
wa Ligi Kuu msimu 2018/2019 yeye ndiye aliyekuwa anasimamia.
Nimekuwa
nafanya hivi ili Taasisi iendeshwe kwa uwazi na kushirikisha kila
mmoja,Na nimeendelea kusisitiza kuwa mapato ya matumizi ya Taasisi
yatatolewa kwenye vyombo vya Habari ili yawe wazi kwa umma.
SEKRETARIETI YA TFF
Toka
tuanze kuunda sekretarieti tumeajiri Wakurugenzi Watatu na Meneja mmoja
na wote hawa waliajiriwa na Kamati ya Utendaji, Ofisi ya Katibu Mkuu
haijawahi kuajiri mfanyakazi hata mmoja kufikia sasa.
Nafasi ambayo haijajazwa ni nafasi ya Katibu Mkuu ambako Ndugu Kidao Wilfred bado anakaimu.
Kwanza
nikiri kazi nzuri inayofanywa na mtendaji mkuu aliyekuwepo katika
kuhakikisha Taasisi inapiga hatua kwa kasi kila ninapokutana na
watendaji wakuu wa FIFA, CAF na CECAFA wamekuwa hawasiti kunimwagia sifa
kwa kuwa na sekretarieti mahiri iliyobadilika katika kufanyia kazi
changamoto za Taasisi.
Raisi
wa FIFA alisema anaona mabadiliko makubwa ya hatua tunazochukuwa,
Lakini Katibu Mkuu wa FIFA alisema nina Sekretarieti ya Vijana wenye
hali, nguvu na maono ya kuipeleka Taasisi mbele huo ndio ujumbe wao.
Nimeyasema
haya kuwahakikishia nikiwa msimamizi wa sekretarieti, mambo yote ambayo
Kaimu Katibu Mkuu amekuwa akiyafanya ni maelekezo yangu au utekelezaji
wa maamuzi halali ya kamati ya Utendaji, Kwahiyo nichukuwe fursa hii
kupongeza kasi ya sekretarieti katika kusimamia mambo mbalimbali.
AJIRA
Katika
kipindi changu cha uongozi (Kamati ya Utendaji) kwa kushirikiana na
ofisi ya Katibu Mkuu tumeweza kupunguza wafanyakazi kutoka Wafanyakazi
44 tuliowakuta wakati naingia madarakani hadi kufikia 21,Ni hatua kubwa
na tunafanya upembuzi makini kabla hatujaanza kuajiri watu tuwe na
mahitaji stahiki.
KATIBU MKUU
Kumekuwa
na maneno mengi juu ya nafasi ya Katibu Mkuu wa Shirikisho, Ndugu zangu
wakati naanza kazi niliona ni muhimu nafasi hii ikaimishwe kwa mtu
anayelijua shirikisho vizuri na ambaye sina shaka na uwezo wake,Sifa
zote hizi alikuwanazo KIDAO WILFRED na wajumbe wa Kamati ya utendaji
chombo ambacho kinahusika nakupitisha kilibariki awe Kaimu Katibui MKuu.
Kutoka
nje ya Ofisi na kukaimu hii siyo mara ya kwanza,wakati Ndugu Tenga
anashinda Uraisi alimuomba Bi.Lina Kessy ambaye alikuwa mtumishi wa
Serikali kuwa Mratibu wa Ofisi, nafasi iliyokuwa kama Mkuu wa
sekretarieti wakati huo.
Hata
wenzetu wa CAF, Rais ndiye anayepeleka jina bila kujali Mchakato
utakavyokuwa kwa maana wanaweza wakatangaza au wasitangaze,na hata
Katiba ya TFF inahitaji Rais wa TFF atoe mapendekezo ya Katibu Mkuu ili
Kamati ya Utendaji ijadili, haya yanafanyika kwa sababu Rais kama
msimamizi wa Sekretarieti anafanya kazi kwa karibu sana na Katibu Mkuu
hivyo FIFA wanahitaji watu hawa wawe wanaoweza kufanya kazi kwa karibu
sana,ndipo Rais wa TFF anapopewa kipaumbele cha mtu wa kufanya naye kazi
kwakuwa ndio nguzo ya Taasisi kwakuwa Rais ndio mkuu wa Taasisi na
Katibu Mkuu ndio mkuu wa Sekretarieti.
Lakini
pamoja na yote hayo bado nilikuwa napeleka ajenda ya Ajira kwenye
Kamati ya Utendaji ili kushauriana njia bora ya kupata Katibu Mkuu kwa
maslahi mapana ya Mpira wa Miguu na siyo mtu.
Niwahakikishie
kikao kijacho cha kamati ya Utendaji kitaamua njia sahihi ya kupata
Katibu Mkuu na tutahakikisha tunakuwa na Katibu Mkuu ndani ya muda mfupi
ujao.
Mipango Mbalimbali
Tumekuwa
katika Ujenzi wa Mipango Mbalimbali kama nilivyoainisha kwenye Ilani
yangu ambapo Katibu Mkuu amekuwa Kiungo muhimu katika kunisaidia kwenye
Ujenzi wa Mipango yangu hiyo lakini kwa bahati Mbaya Kaimu Katibu Mkuu
Kidao amekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kuandamwa na Maneno na
Vitendo vinavyolenga na kufanikisha kumkwamisha na kumkosesha mazingira
bora na rahisi ya kufanyia kazi zake na hivyo imekuwa ni atahri kwa TFF
kwa Baadhi ya Mipango yake kuwa inakwama kutoka Mpaka sasa na hiyo ni
athari kwa Mpira wetu kwa Ujumla.
Ndugu zangu jambo la pili ambalo nimeona niligusie ni jinsi vyombo vya maamuzi vya TFF vinavyofanya kazi,
Ndugu
waandishi, TFF inafanya kazi kwa mujibu wa Katiba yake ya mwaka 2013 na
kufanyiwa marekebisho mwaka 2015. Katiba hii inataja Kamati ya Utendaji
itaundwa na Wajumbe wafuatao;
1. Rais
2. Makamu wa Rais
3. Wajumbe 13 kutoka kanda zilizotajwa ibara 32 ya katiba ambazo ni Kanda namba 1-Kagera na Geita
Kanda namba 2- Mara na Mwanza
Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu
Kanda namba 4- Arusha na Manyara
Kanda namba 5- Kigoma na Tabora
Kanda namba 6- Katavi na Rukwa
Kanda namba 7- Mbeya, Iringa na Songwe
Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma
Kanda namba 9- Lindi na Mtwara
Kmada namba 10- Dodoma na Singida
Kanda namba 11- Pwani na Morogoro
Kanda namba 12- Kilimanjaro na Tanga
Kanda namba 13- Dar es Salaam
4. Wajumbe wawili wanowakilisha vilabu vya Ligi Kuu
5.Mwenyekiti wa Chama cha Soka ya Wanawake.
6. Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba
7. Wajumbe wawili wa kuteuliwa na Rais wa TFF.
Rais
wa TFF amepewa nafasi za kuteua wajumbe wawili wa kamati ya Utendaji
ili kumsaidia kufanya kazi na watu ambao wanajua muelekeo wake lakini
ambao anaamini watamsaidia kwenye maeneo mbalimbali katika Taasisi.
Kamati
ya Utendaji inafanya kazi na vyombo mbalimbali ambavyo ni Kamati
ndogondogo, Bodi ya Ligi na Kamati za Kisheria pamoja na Kamati za
Uchaguzi.
Kamati Ndogondogo;
- Fedha na Mipango
- Mashindano(Kamati ya Tuzo na Soka la Ufukweni)
- Ufundi na Maendeleo
- Vijana
- Wanawake
- Waamuzi
- Katiba, Sheria, na Hadhi za wachezaji.
- Tiba
- Ukaguzi (ambayo yenyewe ni kama Kamati huru)
Kamati za Kisheria;
- Nidhamu
- Rufani ya Nidhamu
- Maadili
- Rufani ya Maadili
Kamati za Uchaguzi;
- Uchaguzi
- Rufani ya Uchaguzi
Ufanyaji
wa kazi wa Kamati hizi umeelezewa katika Katiba ya TFF kwa maana Kamti
za Kisheria zinajitegemea huwa haziingiliwi kwenye maamuzi yake.Ingawa
vikao vyake vyote huwa vinaratibiwa na ofisi ya Katibu Mkuu.
Kwahiyo
maamuzi ya Kamati hizi huwa ni ya kujitegemea hivyo watu wote ambao
wamekuwa wanahukumiwa na Kamati hizi ni vyema wakawa wanajua utaratibu
wa Kamati zinavyofanya kazi.Na mimi binafsi nimeendelea kuheshimu Kamati
zifanye kazi bila kuingiliwa na mtu yoyote vile.
Ndiyo
maana wakati nachaguliwa niliahidi kusimamia Taasisi kwa uadilifu
mkubwa bila kumuonea aibu mtu yeyote, wala kumuogopa mtu na hii ni
katika kuunga mkono juhudi za Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya kupambana na uchafu wa aina zote katika serikali,Nami nimeamua
kusafisha Taasisi kama nilivyoahidi wakati wa Kampeni za uchaguzi
ulioniweka madarakani,niseme wazi hakuna mtu asiye muadilifu atabaki
katika mpira,Na nimpongeze Kaimu Katibu Mkuu wangu kwa kusimamia kwa
ujasiri mkubwa usimamiaji wa maagizo yote halali ya Kamati
mbalimbali,Amekuwa anasimamia bila uoga bila kujali anavyosakamwa kwangu
linanipa faraja sana.
Tumekuwa
tunachukuwa hatua katika kila eneo tumeshaanza kuchukuwa hatua kwa wizi
wa Mapato ya milangoni, kuna viongozi wamefungiwa,hatukuishia hapo
tayari viongozi walioghushi leseni za usajili wamefungiwa,Hiyo yote
ikiwa ni kuonesha sina masihara hata kidogo kwenye kuhakikisha mpira
unakuwa sehemu ya watu waadilifu.
FIFA
walituma Timu ya Uchunguzi(Investigation Team) kuangalia yale yote
yaliyofanyika toka mwaka 2013 mpaka mwaka 2017,Timu ilikaa nchini kwa
takribani wiki mbili ikifanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Katibu
Mkuu,Yaliyogundulika yameacha doa kubwa na walitoa Ripoti na Maelekezo
ya mambo ya kuyafanyia kazi na ya kuchukulia hatua.
Masharti
yote haya yaliambatana na kuzuiwa kwa fedha zetu za miradi nia na
wenzetu wachache, Lakini tumekosa pesa zinazoitwa Operation Cost ikiwa
ni shinikizo la Dola Milioni Tatu ambazo tulipaswa kulipwa toka mwaka
2015-2018.
Karibia
nchi zote Duniani zimenufaika kwa kupata pesa hizi, isipokuwa Tanza
kuhakikisha tunatekeleza masharti ya FIFA, Hivyo tulipopata ripoti
tumeamua kutekeleza kwa asilimia mia moja maagizo yote ya FIFA. Haya
yanayotokea ni Miongoni mwa Matokeo ya Utekelezaji wa Taarifa za
Wakaguzi wa TFF na Wakaguzi na Timu ya Uchunguzi kutoka FIFA. Jambo hili
limepitia Hatua stahiki kwa Mujibu wa Taratibu zinazohusiana na Taarifa
za kiUkaguzi na wahusika wameshirikishwa ipasavyo na Utetezi wao
walipeleka kwenye Kamati husika ya Ukaguzi miezi iliyopita baada ya
kutakiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu.
Niseme
tu unaposafisha Taasisi kuna gharama zake TFF inahitaji Kuungwa Mkono
zaidi kwa Hatua Madhubuti inazochukua za Kujisafisha na Kusonga Mbele.
Katika
VITA hii ya Kupambana na Udhalimu kwenye Mpira wetu Hatutarudi Nyuma,
Tutapambana bila hofu wala woga almuradi Hakuna dhulma wala Uonevu wala
Upendeleo kwa yeyote. Na Nitoe wito kama kuna Kiongozi au Mdau yoyote
anayejua ana Pesa za TFF kinyume cha Utaratibu Natoa WITO Ajisalimishe
Mwenyewe.
Ahsanteni kwa kunisikiliza naamini mtaniunga mkono ili kuusogeza mbele Mpira wa Tanzania.
Mwisho
niwakumbushe TFF inaendelea na maandaalizi ya Matayarisho wa AFCON U
17,2019 .Timu ya ukaguzi ya CAF itakuja mwezi wa Tano, tumekuwa
tunalifanyia kazi kwa ukaribu na serikali kuhakikisha changamoto za
viwanja vitavyochezea mashindano pamoja na viwanja vya mazoezi vinakuwa
tayari kwa wakati.Tutaendelea kulitolea ufafanuzi kila wakati.
No comments:
Post a Comment