Wanaume
18 kati ya waliofika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuhojiwa
kuhusu kutelekeza watoto wamekubali kupimwa vinasaba (DNA) na Mkemia
Mkuu wa Serikali, taarifa iliyotolewa jana na Paul Makonda ilisema.
Makonda
alisema hatua hiyo imefikiwa na wanasheria na maofisa ustawi wa jamii
baada ya kuhoji wanaume waliodaiwa kuwatelekeza watoto, katika
malalamiko yanayoendelea kutolewa na wanawake kuanzia Jumatatu katika
ofisi hizo, Ilala.
Mkuu wa Mkoa Makonda alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea maendeleo ya zoezi linalomalizika leo.
"Jumla
ya wanaume 18 ambao walibisha kuwa watoto sio wao wamekubali kwenda
kupimwa DNA kwa Mkemia Mkuu ili kupata uthibitisho wa uhalali wa mzazi
na hao ni kati ya wanaume 198 walioitikia wito na kuja ofisini kwangu,"
alisema Makonda.
Kadhalika,
alisema kati ya wanaume 198 waliofika katika ofisi hizo baada ya
kuandikiwa barua za wito, 179 walikubaliana na wanawake waliozaa nao
mikakati ya kulea watoto husika.
"Familia
179 zimefikia muafaka," alisema Makonda na "haya ni mafanikio makubwa.
Kama watu waliokuwa hawahudumii familia na leo hii wamekubali kuhudumia
na kurudi nyumbani kwa amani, kazi hii imezaa matunda."
Makonda
alisema kati ya wanaume 198 waliofika katika ofisi hizo kutafuta
mwafaka, 19 kati yao mashauri yao yamepelekwa mahakamani ili kutafuta
suluhu.
"Kazi
inaendelea vizuri, tunaona mafanikio kwa sababu wanawake waliojitokeza
ni wengi wanaokosa huduma kutoka kwa wanaume zao," alisema. "Wanaume
waliopewa barua za wito nao wamekuja wakasilikizwa na mwafaka
ukapatikana."
Pia
alisema wanawake 1,498 wamejitokeza katika siku tatu kwa ajili ya kutoa
malalamiko yao na kupewa msaada wa kisheria.Makonda alisema kutokana na
kuwapo kwa idadi hiyo kubwa ya wanawake, wameongeza wanasheria 200 na
maofisa ustawi wa jamii 60 na kusababisha kuwapo kwa watoa huduma 378.
"Kwa
sababu ya mwitikio mkubwa wa wanawake, tumelazimika kuongeza wanasheria
na maofisa ustawi wa jamii ili kazi hii ifanyike kwa haraka," alisema
Makonda.
Aidha,
Makonda alisema baada ya kusikiliza wanawake waliotelekezwa, kanzia
Jumatatu itakuwa zamu ya wanaume ambao wameandikiwa barua za wito.
"Ingawa
wapo baadhi ya wanaume ambao wameandikiwa barua za wito na wameshakuja
kusikiliza walichoitiwa, kuanzia Jumatatu itakuwa ni siku ya
kuwasikiliza baada ya kuwasikiliza wanawake," alisema Makonda.
Alisema
wanaume ambao wamepewa wito huo wanatakiwa wajitokeze kusikiliza na
endapo watakaidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Makonda
pia aliwataka wanawake na wanaume wenye matatizo ya kutelekezewa watoto
kweli wajitokeze katika ofisi hizo ili wapate msaada wa kisheria bure
badala ya kuandika kwenye mitandao ya kijamii.
"Kama
kweli mtu ana matatizo ni wajibu wake kuja hapa ili asikilizwe na
kupatiwa msaada bure badala ya kuandika kwenye mitandao ya kijamii
ambako hakuna majibu," alisema Makonda.
Leo ni siku ya mwisho ya kutoa msaada wa kisheria kwa wanawake ambao walitelekezewa watoto na wanaume waliozaa nao.
No comments:
Post a Comment