Wakati
ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ukiendelea, Shirika la Reli Tanzania
(TRC) limeagizwa kuwasilisha kwa maandishi mkakati wa upatikanaji wa
umeme wa uhakika wa kuendesha treni hiyo kwa Kamati ya Bunge, Uwekezaji
na Mitaji ya Umma (PIC) kabla ya Mkutano wa Bunge la Novemba.
Wabunge hao wametoa agizo hilo kwa TRC kutokana na wasiwasi wao kuhusiana na upatikanaji wa umeme wa kutosha.
Agizo
hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa kikao cha kamati hiyo, Janet Mbene,
baada ya shirika hilo kuwasilisha majibu ya hoja ambazo kamati
iliziagiza mara ya mwisho walipokutana na utekelezaji wa majukumu yao
tangu ilipoundwa TRC.
Mbene
alisema TRC ambayo ndiye msimamizi wa ujenzi huo inatakiwa ioneshe
mkakati wake wa kuanza kujiandaa kuhusu umeme utakaotumika kwenye treni
hiyo, watumishi watakaofanya kazi, ulinzi na vitu vyote vinavyoendana na
uendeshaji wa treni hiyo.
“Treni
ya SGR itatumia umeme, hatujaona popote wapi mmeanza mazungumzo na
Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) kujua umeme utapatikana vipi na kwa
gharama zipi, lazima hivi vitu sasa hivi mvitazame, msisubiri hadi treni
ifike na reli imekamilika ndio mnaanza kufanya kazi,” alisema Mbene.
Mbene aliwataka kuwasilisha mkakati wa uboreshaji gani utafanyika kwa reli iliyopo wakati wakiwa wanasubiri SGR.
“Mpango
uliopo wa kujenga SGR mpaka Makutupora, lakini reli hii inapaswa kufika
Kigoma na Mwanza kwa hiyo tumeagiza waje na mchanganuo unaoonesha jinsi
gani hii reli itafika Kigoma na Mwanza,” alisema zaidi Mbene.
Mwenyekiti
huyo alisema shirika hilo linaweza kukopa au kuingia ubia kama njia
ambazo zipo wazi kwao zitawafanya wawe na fedha za kutosha za kufikisha
reli mwisho badala ya kusubiri kutoka serikalini.
“Tayari
wanasema kuna wawekezaji wameonyesha nia ya kuwekeza na wapo tayari
kuwekeza maeneo ya hiyo reli, sasa tunataka watuletee tuone je, kwa
kuwatumia hao huo mpango wa ubia unaweza kuwa na manufaa badala ya
kusubiri serikali pekee iwekeze,” alisema.
Pia
Mbene alisema mfuko unaotokana na uagizwaji wa bidhaa nje ambapo
asilimia 1.5 ya fedha huingia moja kwa moja kwenye miundombinu ya reli
ni vyema fedha nyingine itumike kuboresha miundombinu ya reli na SGR
iliyopo kwa kuweka mgawanyo sawa.
Kadhalika,
alisema kuna fedha zimetoka Benki ya Dunia Dola za Marekani milioni 300
kwa ajili ya ukarabati wa reli ambapo unahusisha madaraja, maeneo ya
madaraja na vipande vya reli.
“Musoma-Bukoba,
Moshi-Tanga, Mtwara-Mchuchuma, Mpanda-Kaliua, sasa vyote hivi ni vya
fedha kutoka benki ya dunia tunachohitaji kujua wana mkakati gani
mbadala wa kuhakikisha kuwa ufanisi hautaathirika na tumeagiza haya yote
yaletwe bunge la mwezi Novemba,” alisema.
Alisema
kumekuwapo na changamoto ya kila mwaka inayojirudia katika kipande cha
reli cha Gulwe hadi Kilosa ambapo mvua zikinyesha reli husombwa na
kusababisha adha kwa wasafiri.
“Tumeona
hii ni kero ambayo inaweza kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, inawezekanaje
kila mwaka wanakuwa na mikakati hafifu, kwa hiyo tumeagiza watuletee
maelezo ya ufumbuzi wa kudumu kwa maeneo korofi ili kupunguza gharama
zinazotokana na ukarabati wa kila siku na usumbufu kwa wananchi
wanaotumia treni,” alisema.
Akijibu
baadhi ya hoja, Mwenyekiti wa Bodi ya TRC, Prof. John Kondoro, alisema
kuna mazungumzo yanaendelea ya upatikanaji wa umeme na vitu mbalimbali
yapo katika maandiko.
Aidha,
alisema ukarabati mwingi unafanyika na maeneo yameainishwa ambapo kuna
baadhi ya njia na madaraja zinakarabatiwa kwa kuwa mtandao wa reli una
jumla ya madaraja 400.



No comments:
Post a Comment