Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameendelea kuwabana polisi
akiwataka kuachana na tabia ya kubambikia raia kesi zikiwamo za
uzururaji na ugaidi.
Lugola
alitoa kauli hiyo Jumatatu jioni baada ya kufanya ziara ya kikazi
katika Chuo cha Taaluma cha Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam na
kuzungumza na maofisa wa chuo hicho na wanafunzi.
Alisema aliamua kufanya ziara hiyo baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa raia kuhusu kubambikwa kesi na askari polisi.
"Miongoni mwa kesi ambazo raia wanalalamikia kubambikiwa sana ni uzururaji na kesi za ugaidi," Lugola alisema.
Waziri
huyo aliongeza kuwa, kuna maofisa wenye vyeo ndani ya jeshi hilo
aliokutana nao lakini kutokana na vitendo vyao amewatilia shaka kama
kweli waliwahi kupitia mafunzo chuoni hapo.
"Kuna
baadhi ya mambo yanayofanyika kule chini ambayo yananishangaza sana,
nimekuwa nikijiuliza jeshi hili ni la weledi na wa kisasa kweli? Yuko
OCS mmoja (Mkuu wa Kituo) kama ninyi, yupo kwenye kituo cha polisi.
"Yeye
kila kukicha asilimia 90 ya watu ambao anawakamata na kuwaweka ndani
wote ni dili analotengeneza yeye, najiuliza ina maana siku hizi
tunakwenda kusoma tuje kutengeneza madili?"
"Moyo
wa kufukuzia madaraka haupo, nimeona umuhimu wa mafunzo haya pengine
mimi nikisema mtabadilika na ninyi wakati mnasoma mtakuja kunikumbuka
siku moja kuwa alikuja waziri akatukumbusha.
"Si
lazima uchafuke mabega upate madaraka, kuna watu wamechafuka mabega
lakini ndiyo hao wa madili... kuna watu hawajachafuka wanafanya kazi
vizuri, wapo huko vituoni."
Waziri
huyo aliwataka maofisa na askari chuoni hapo kuhakikisha wanatumia
mafunzo hayo kulinda usalama wa raia na siyo kuwakandamiza kwa
kuwabambikia kesi mbalimbali.



No comments:
Post a Comment