Faru
maarufu anayejulikana kwa jina la Fausta amezua gumzo bungeni baada ya
Mbunge wa Viti Maalumu, Suzana Mgonokulima, kuhoji ni kwa nini serikali
inamhudumia faru huyo kwa gharama kubwa wakati hazalishi kutokana na
kuwa mzee.
“Serikali
inamhudumia Faru Fausta kwa gharama ya Sh milioni 64 kwa mwezi, lakini
serikali haiwezi kuhudumia mwananchi aliyezeeka ambaye hawezi kufanya
shughuli yoyote ya kujikimu na maisha na hana mtu wa kumsaidia, je ni
kipi muhimu zaidi kati ya Faru Fausta au mwananchi mzee asiyeweza
kufanya lolote na hana wa kumsaidia,” amehoji mbunge huyo.
Akijibu
swali hilo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema
faru huyo amekuwapo katika Hifadhi ya Ngorobgoro tangu mwaka 1965 ambapo
kwa sasa ndiye faru mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani.
“Kutokana
na uzee, Faru Fausta alijeruhiwa na fisi Septemba mwaka juzi, hivyo
kulazimu atunzwe kwenye kizimba kwa ajili ya uangalizi maalumu ambao
unahusisha matibabu na chakula, hivyo gharama iliyokuwapo kipindi hicho
ilitokana na hali ya dharura iliyohitajika ikiwamo miundombinu, ulinzi,
matibabu na malisho ambayo matumizi yote hayo kwa mwezi yalikuwa Sh
milioni 1.4 kwa sasa hali yake inazidi kuimarika na gharama imepungua
hadi Sh 285,000 kwa mwezi.
“Hata
hivyo, faru huyo si kwamba ni muhimu kuliko wazee bali uamuzi wa
kumtunza kwenye kizimba ulifanyika kwa lengo la kunusuru maisha yake ili
aendelee kuwa kivutio cha utalii na kuingiza fedha za kigeni nchini,”
amesema.
Hata
hivyo, majibu hayo hayakumridhisha mbunge suzana ambaye katika swali
lake la nyongeza alihoji tena umuhimu wa faru huyo ambaye hata hivyo
amefungiwa watalii watamuonaje na kwamba umuhimu wake ni zaidi ya wazee
waliopigania nchi na kuleta amani lakini hawatunzwi na serikali.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri Hasunga amesema faru huyo anahifadhiwa
kutokana na umuhimu wake na jinsi alivyoliingizia taifa fedha nyingi za
kigeni na wengi wanataka kujua ataishi miaka mingapi ambapo sasa hivi
ana miaka 53.
Hata
hivyo, hali hiyo ilimuibua Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile ambaye amesema kwa
mujibu wa sera ya afya serikali inatambua wazee ambapo imeweka utaratibu
wazee zaidi ya miaka 60 wanapata matibabu na wanapata kipaumbele kwenye
huduma ya afya ambapo mapato yanayopatikana katika Sekta ya Utalii
ndiyo hayo hayo yanakwenda kuhudumia wazee hao.
No comments:
Post a Comment