Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
*Wagonjwa 45 wahudumiwa, wagharimu Tshs. 360 Mil. badala ya Tshs. 4.320 Bil kama wangeenda nje ya nchi
*Mmoja agharimu Tshs. 8 Mil. badala ya Tshs. 96 Mil. nje ya nchi
Hospitali
ya Taifa Muhimbili imeanzisha kwa mara ya kwanza hapa nchini utoaji wa
huduma za tiba radiolojia (Interventional Radiology) ambapo kabla ya
uanzishwaji wake wagonjwa waliokuwa wanahitaji huduma hizi walikuwa
wakienda nje ya nchi.
Akizungumza
na wanahabari jijini Dar es Salaam wakati akielezea kuanzishwa wa
huduma hiyo, Mkurugenzi wa wa huduma za Tiba Shirikishi Dkt. Praxeda
Agweyo amesema kuwa tiba hiyo inahusisha utalaam wa kutumia vifaa vya
radiolojia kama X-Ray, MRI, CT-Scan na Ultra-Sound kutibu moja kwa moja
ugonjwa au kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi.
Amesema
kuwa huduma ambazo zimeanza kutolewa kupitia njia hiyo kwa sasa ni
kuondoa uvimbe kwenye sehemu ya kinywa, uso na shingoni (sclerotherapy
for haemangioma and lymphangioma), kuweka mirija kwenye figo ambazo
mirija ya kutoa mkojo imeziba (nephrostomy tube placement), kuzibua
mirija ya nyongo iliyoziba (percutaneous trans hepatic biliary drainage)
na kuzibua mirija ya uzazi iliyoziba (fallopian tube recanalization).
Tiba
nyingine ni kunyonya usaha ndani ya tumbo (abscesses drainage).
Ameongeza kuwa wastani wa mgonjwa mmoja kutibiwa uvimbe kwenye sehemu ya
kinywa (sclerotherapy for haemangioma) inagharimu kiasi cha Tshs. 2
mil. ambapo kutokana na ugonjwa huo mgonjwa anahitaji kutibiwa hatua nne
ili kukamilisha mzunguko wa tiba hiyo sawa na Tshs. 8 mil.
"Mgonjwa
kama huyo alipokuwa akienda nje ya nchi ilikuwa inagharimu kiasi cha
Tshs. 24 mil. kwa kila hatua moja sawa na Tshs. 96 mil. kwa hatua zote
nne," amesema Dkt. Ongweyo. Tangu kuanzishwa kwa huduma hizi Novemba
2017, jumla ya wagonjwa 45 wamenufaika kwa gharama ya Tshs. 360 mil.
sawa na Tshs. 8 mil. kwa kila mgonjwa. Kama wangeenda nje ya nchi
ingeigharimu Serikali kiasi cha Tshs. 4.320 Bil. sawa na Tshs. 96 mil.
kwa kila mgonjwa.
"Tunamshukuru
Mungu mpaka sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili imeokoa kiasi cha Tshs.
3.96 Bil. kwa kutoa huduma hiyo hapa nchini. Uwepo wa huduma hii hapa
nchini utasaidia wananchi wengi kunufaika na hatimaye kupunguza mzigo wa
kulipa fedha nyingi kwa matibabu huko nje," amesema Dkt. Ogweyo.
Kabla
ya uanzishwaji wa huduma hizi hapa nchini, vifaa vilivyopo katika Idara
ya Radiolojia kama vile X-Ray, MRI, CT-Scan na Ultra-Sound vilikuwa
vinatumika kufanya uchunguzi tu wa magonjwa lakini sasa vinatumika
kutibu pia.
"Tunashukuru
uongozi mzima wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kuweza kuwapa
madaktari wao mafunzo zaidi na kuweza kuwa wa kisasa zaidi, tulipopata
mafunzo kwa madaktari wa hospitali ua Kenyatta walitufungua mengi na
sasa nasi tunaweza na tunaokoa fedha za serkali," amesema Dkt. Ogweyo.
No comments:
Post a Comment