Sakata
la makontena 20 yaliyoko Bandari ya Dar es Salaam kwa jina la Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda limemwibua waziri wa zamani katika
Serikali ya awamu ya nne, Profesa Mark Mwandosya akikumbushia misingi ya
utawala bora.
Makontena hayo yaliyokwama bandarini baada ya Makonda kushindwa kulipa kodi ya Sh bilioni 1.2, kwa mara ya pili juzi yalishindwa kuuzwa kwa mnada baada ya wanunuaji kushindwa kufikia bei.
Juzi,
Profesa Mwandosya aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter,
akisema alivyofundishwa misingi ya utawala bora, mkuu wa nchi akimkosoa
mtumishi hadharani, anapaswa kuandika barua ya kujiuzulu.
Ingawa
hakumtaja Makonda moja moja, lakini ni wazi kuwa alimlenga mkuu huyo wa
mkoa wa Dar es Salaam, kwa kuwa ni siku chache tu baada ya Rais
Magufuli kumkosoa Makonda hadharani na kumtaka alipe kodi hiyo.
“Nilifundishwa
misingi ya utawala, mkuu wa nchi akimkosoa mtumishi hadharani,
unapeleka barua ya kujiuzulu ili kulinda heshima yake na kwa kufanya
hivyo unajijengea heshima mbele ya umma. Nikiri kwamba huenda misingi
hiyo imepitwa na wakati,”aliandika Profesa Mwandosya.
Jumapili ya Agosti 26 mwaka huu, Makonda alifanya ibada maalumu ya kumwomba Mungu ili wanaofanya mnada wasipate wateja.
“Amelaaniwa
mtu yule atakayenunua furniture (samani) za walimu. Nimefanya ibada
maalumu ya kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa sababu naamini
Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wanaofanya
kazi katika mazingira magumu ikiwa ni jitihada zangu binafsi." Alisema Makonda
Kauli
hiyo ya Makonda ilimwibua Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango
siku moja baadaye, aliyeapa kusimamia sheria na kuhakikisha makontena
hayo yanapigwa mnada
No comments:
Post a Comment