Rais
Magufuli amekataa ombi la Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina
ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa mkoani Simiyu la kutaka jimbo lake liwe
halmashauri.
Rais Dk.Magufuli alisema kuanzisha maeneo mapya ya utawala kumekuwa kukiongeza gharama za uendeshaji.
Alisema ni bora fedha hizo akazitumia kuwaletea wananchi maenedeleo kuliko kuongeza halmashauri.
Rais
Magufuli alitoa kauli hiyo jana katika mji wa Mwandoya wilayani Meatu
aliposimama kusalimia wananchi, wakati wa ziara ya kukagua shughuli za
maendeleo.
Awali
Mpina alimwomba Rais Dk. Magufuli kuwapatia halmashauri wananchi wa
Kisesa kutokana na kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kiutawala.
“Wananchi wa Kisesa wamekuwa wakipata wakati mgumu kwenda mji wa Mwanhunzi ambapo kuna ofisi za halmashuari.
“Wilaya
ya Meatu kuna majimbo mawili na yote yanategemea halmashauri moja. Hawa
wananchi mheshimiwa Rais, wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya 100
kwenda makao makuu ya mkoa, kilomita 60 kwenda makao makuu ya
halmashauri.
“Mheshimiwa
Rais umbali huo wote ni mrefu, sisi hatuombi wilaya, tunaomba utupatie
halmashauri ya kwetu sisi wenyewe,” alisema waziri huyo.
Mpina alisema uwezo wa kujiendesha kama halmashauri upo, kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya watu zaidi ya 170,000.
Alisema
mbali na idadi ya watu, Jimbo la Kisesa lina uwezo wa mapato, kwani
limekuwa likikusanya zaidi ya Sh bilioni 2 kwa mwaka pamoja na kuwapo
kwa miundombinu mingine ya kutosha kuwa halmashauri.
Huku
akishangiliwa na umati mkubwa wa wananchi, Waziri Mpina alisema
kupatikana kwa halmashauri kutasababisha wananchi wa jimbo hilo kupata
maendeleo kwa haraka.
Akizungumzia
ombi hilo, Rais Magufuli alisema kwa sasa hawezi kuanzisha maeneo mapya
wakati wananchi wengi bado ni maskini na badala yake atahakikisha
anawaletea maendeleo na si kuwaletea halmashauri.
Rais
Magufuli alilazimika kutoa mifano mbalimbali ya majimbo yenye maeneo
makubwa, lakini kuna halmashauri moja, ambapo alitolea mfano wa
halmashauri ya Chato ambayo alieleza kuwa idadi ya watu ni zaidi ya
400,000.
“Kuna
majimbo mengi tena makubwa zaidi ya hili na yana idadi kubwa ya watu
kuliko hapa Kisesa, kuna halmashauri moja, siwezi kuleta halmashauri
wakati najua itaongeza gharama za uendeshaji,” alisema Rais Magufuli.
“Kupanga
ni kuchagua, niache nishughulikie masuala ya barabara, umeme, maji na
afya, siyo kuwaletea halmashauri, haya maombi yenu yatakuwa baadaye
lakini siyo sasa hivi, siwezi kuleta halmashauri, nitaleta
maendeleo,”alisema Rais Maguli.
Alisema hawezi kuwadanganya kuwa atawapatia halmashauri wakati jambo hilo hawezi kulifanya kwa sasa.
No comments:
Post a Comment