Wizara
ya Mifugo na Uvuvi inatekeleza mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya
mifugo unaotarajiwa kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa
kutoka asilimia 6.9 hadi 9%.
Naibu
Waziri wa Wizara hiyo, Abdallah Ulega amesema bungeni jijini Dodoma
kuwa, utekelezaji wa mkakati huo pia unatarajiwa kukuza sekta ya mifugo
kutoka asilimia 2.8 hadi 5.2%.
Wakati
anajibu swali la Mbunge wa Kibaha Mjini, Silyvester Koka, Ulega
amesema, mkakati huo una lengo la kupunguza na kuboresha mazingira
rafiki na endelevu katika uzalishaji mifugo yenye tija kwa kuzalisha
mitamba milioni moja kwa mwaka.
Wabunge
wameelezwa kuwa mitamba hiyo itapatikana kutoka makundi ya ng'ombe wa
asili kwa kufanya uhimilishaji. Koka alitaka kufahamu Serikali ina
mpango gani kuboresha bidhaa za nyama nchini pamoja na mazao mengine
yatokanayo na mifugo.
Ulega
amesema, mkakati wa kuendeleza sekta ya mifugo utaimarisha upatikanaji
wa uhakika wa maji, malisho na vyakula bora vya mifugo, utahamasisha
matumizi ya teknolojia za ufugaji wa kisasa, utaboresha afya, masoko,
biashara na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo.
Amesema,
mkakati huo utaongeza uzalishaji mazao ya mifugo ikiwemo idadi ya
ng'ombe wa maziwa kutoka 789,000 hadi milioni tatu, utaongeza uzalishaji
maziwa kutoka lita bilioni 2.4 hadi lita bilioni 3.8 kwa mwaka.
Kwa
mujibu wa Ulega, mkakati huo pia utaongeza uzalishaji wa nyama kutoka
tani 679,992 hadi tani 882,100, utaongeza uzalishaji ngozi za ng'ombe,
mbuzi na kondoo kutoka futi za mraba milioni 89 hadi futi za mraba
milioni 98.9 na utaongeza uzalishaji mayai kutoka mayai bilioni 3.2 hadi
mayai bilioni 6.4.
"Pia,
mkakati unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za ugani, kuongeza
uzalishaji wa chanjo za mifugo zinazozalishwa hapa nchini, kuongeza
usindikaji wa mazao ya mifugo, pamoja na kuongeza usambazaji wa
teknolojia za ufugaji bora ili kufikia wafugaji wengi zaidi"amesema
Ulega.
No comments:
Post a Comment