Serikali
imeahidi kuendelea kuwezesha vituo vyake vya utafiti kote nchini kwa
lengo la kuongeza uzalishaji wa aina mpya za mbegu bora za mazao mbali
mbali.
Kauli
hiyo imetolewa na Mhe Dkt Charles Tizeba Waziri wa Kilimo, wakati
akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa mbegu ambapo ni mjumuiko wa
Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Mbegu (TASTA), TOSCI, USAID East Africa
Trade Investment Hub, AGRA-MIRA Project, AATF, ASA na TPRI kwa
kushirikiana na wizara ya Kilimo na wadau wengine wa maendeleo
unaofanyika katika Ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha.
Alisema
kuwa katika kuhakikisha kuwa Wizara ya kilimo inafikia hatua ya kuwa na
uzalishaji Wa aina mpya za mbegu bora za Mazao mbalimbali tayari
serikali imechukua hatua ya kuanzisha Taasisi ya Utafiti Wa kilimo -
TARI kwa lengo la kuboresha utendaji wa kitafiti ili kuleta tija katika
ugunduzi wa aina mpya za mbegu.
Alisema
kuwa TARI itasaidia kuongeza uzalishaji wa mbegu bora hapa nchini na
hivyo kuwa na matokeo chanya ya uhakika wa chakula katika ngazi ya kaya
na Taifa kwa ujumla pia kuongeza kipato kutokana na ziada.
Dkt
Tizeba alisema kuwa Mpango wa Kuendeleza sekta ya Kilimo awamu ya pili –
ASDP II ambao Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John
Pombe Magufuli ameuzindua hivi karibuni unasisitiza masuala ya
uendelezaji wa kilimo chenye tija, Kilimo biashara chenye kuboresha
mapato ya mkulima na kilimo kinachomhakikishia mkulima usalama wa
chakula na lishe.
"Haiwezi
kuwa rahisi kuongeza uzalishaji wa kilimo hapa nchini kama msingi wa
kilimo ambao ni uzalishaji wa mbegu bado tutakuwa tumeuacha nyuma pasina
kuweka msisitizo hapo, hivyo tunapaswa kutazama upya namna bora ya
kupunguza gharama ya mbegu" Alikaririwa Mhe Dkt Tizeba na kuongeza kuwa
"Baada
ya serikali kujitoa katika uendeshaji wa biashara mbalimbali na
kuruhusu sekta binafsi kufanya biashara, hii ilitoa fursa kwa sekta
binafsi kushiriki katika tasnia mbalimbali ikiwemo hii ya mbegu, lengo
kuu la dhana hii ya ushirikishaji wa sekta binafsi na ile ya umma (PPP)
ni kuwezesha na kuhakikisha kwamba maslahi mapana ya wakulima yanalindwa
na mazingira ya biashara yanaboreshwa ili wakulima na sekta binafsi
wote wafaidike na jitihada wanazozifanya"
Waziri
Tizeba aliongeza kuwa Ili kutekeleza lengo la kuongeza tija na
uzalishaji katika sekta ya mbegu, Wizara ya Kilimo kupitia Sheria ya
Mbegu ya Mwaka 2003, imeweka mifumo mbalimbali ya namna ya kutoa na
kufikisha huduma kwa wakulima kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa
lengo la kuboresha huduma hizo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa maendeleo
ya wakulima.
Alizitaja
jitihada hizo kuwa ni katika kutekeleza majukumu ya pamoja katika ubia
baina ya sekta ya umma na ile ya binafsi. "Lakini kwa bahati mbaya
juhudi hizi hazijazaa matunda yaliyotarajiwa na ndiyo maana mpaka sasa
bado tunakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uzalishaji mdogo wa
mbegu, uwepo wa mbegu zisizokidhi viwango vya ubora sokoni na kutegemea
mbegu za kuagizwa kutoka nje. Hali hii tunatakiwa kuondokana nayo na
kuhakikisha tunazalisha mbegu za kutosha mahitaji ya ndani na ziada
kuuza nje" Alisistiza Dkt Tizeba
Aidha,
alidema juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika kati ya Serikali na
Sekta binafsi katika kupambana na uwepo wa mbegu zisizokidhi viwango vya
ubora sokoni. Miongoni mwa juhudi hizo ni kuweka karatasi yenye maelezo
na utambulisho ‘label’’ katika vifungashio vya mbegu. "Hii ni sehemu ya
utekelezaji wa Sheria ya Mbegu ya mwaka 2003 ambapo utekelezaji wake
umekuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na malalamiko ya
wafanyabiashara kudai kuwa hizo ‘lebel’ zinaongeza gharama. Hivyo
napenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha wadau wote wa sekta ya mbegu
kuwa hilo ni takwa la kisheria hivyo ni budi sote tulizingatie" Alisema
MWISHO.
No comments:
Post a Comment