Serikali
imesema inaangalia uwezekano wa kuondoa kodi ya vifaa vya uongezaji
thamani madini ikilenga kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani
madini kufanyika nchini.
Hayo
yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati akijibu
swali la mwanafunzi wa Kituo Cha Jemolojia Tanzania (TGC) Rojer Mpele
aliyeiomba Serikali kupitia Naibu Waziri kuangalia namna ya kupunguza
kodi ya vifaa hivyo ili kuwasaidia wanafunzi wanaojifunza ukataji na
ung’arishaji madini katika kituo hicho kuweza kujiajiri baada ya
kuhitimu .
Nyongo
ameongeza kuwa, tayari Serikali imeanza kufanya taratibu za kupeleka
maombi kuhusu jambo hilo katika Mamlaka husika ili liweze kufanyiwa
kazi kwani litahamaisha uwekezaji wa viwanda vya uongezaji thamani
madini nchini ikiwemo kuongeza wigo wa ajira na mapato kupitia sekta ya
madini.
Naibu
Waziri Nyongo amekitembelea kituo hicho kilichopo jijini Arusha kwa
lengo la kujifunza shughuli zinazofanyika kituoni hapo. Kituo cha TGC
kipo chini ya Wizara ya Madini, kinatoa mafunzo ya ukataji na
ung’arishaji madini ya vito lengo likiwa ni kuongeza thamani madini.
Ameongeza
kuwa suala la uongezaji thamani madini nchini ni jambo ambalo ni
kipaumbele cha serikali kutokana na Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya
Mwaka 2010 na Maboresho yake ya Mwaka 2017 na kwamba tayari serikali
imezuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi na badala yake
inahamasisha shughuli hizo kufanyika hapa hapa nchini kwa kuwa,
zitawezesha kuleta ujuzi, ajira, mapato zaidi ya serikali na kuyaongezea
thamani madini hayo nchini kabla hayajasafirishwa nje ya nchi.
“Bado
Wizara inaweka msisitizo wa shughuli za uongezaji thamani zifanyike
hapa nchini. Kwa hiyo napenda kuwaambia ninyi vijana mnajifunza kitu
ambacho ni kipaumbele kwa wizara na serikali,” amesisitiza Naibu Waziri.
Aidha,
Naibu Waziri amesema kuwa, serikali kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu
wa Rasilimali Madini (SMMRP) unaotekelezwa chini ya wizara kutokana na
mkopo wa Benki ya Dunia, tayari umeagiza vifaa mbalimbali kwa ajili ya
kuanzisha karakana ya shughuli za uongezaji thamani madini katika kituo
hicho, karakana hiyo inalenga kutumiwa na wahitimu wa kituo husika ili
kwawezesha kujiajiri pindi wanapohitimu mafunzo yao.
“Watakaohitimu
hapa watalipia gharama ndogo sana za mashine watakazokuwa wakizitumia
kufanya kazi zao katika karakana hiyo. Lakini pia, ili kuboresha
shughuli za karakana hiyo, tutaendelea kujifunza kwa nchi nyingine namna
wanavyoendesha karakana zao,” ameongeza Nyongo.
Katika
jitihada za kuendelea kukiboresha kituo husika, Naibu Waziri Nyongo
amemtaka Mratibu wa Kituo hicho, kuandaa Mpango Mkakati wa namna ya
kukiboresha na kukitanua kituo hicho ili kiweze kuwa bora na mfano kwa
nchi nyingine barani Afrika.
“
Imefika wakati ambapo tunataka TGC kuwa chombo ambacho kinatoa ujuzi wa
hali ya juu katika uongezaji thamani madini. Lazima tutoe mafunzo kwa
vijana wa kitanzania na tuendelee kuangalia namna ya kuleta ujuzi au
kwa kuwapeleka vijana wetu kujifunza kwa wenzetu na baadaye wawe
wakufunzi katika kituo hiki.
Vilevile,
Naibu Waziri Nyongo amesisitiza kuwa, Serikali kupitia wizara ya Madini
itaendelea kusimamia kwa karibu kuhakikisha kuwa inatekeleza na
kutimiza malengo ya uanzishwaji wa kituo hicho. “Lazima ifike mahali
kituo kitoe mafunzo kwa jinsi ilivyokusudiwa, ameongeza Nyongo.
Kwa
upande wake, Kaimu Mratibu wa Kituo cha TGC, Eric Mpesa amesema kuwa,
kituo hicho ni kituo pekee Afrika Mashariki kinachoendeleza taaluma ya
uongezaji thamani madini ya vito na miamba.
Pia,
amesema kuwa, kituo kinakusudia kutoa mafunzo ya Diploma ya Gem Jewelly
technology ambapo mhitimu katika mwaka wa Kwanza atapatiwa cheti cha
NTA Level 4, mwaka wa pili NTA Level 5 na mwaka wa tatu NTA Level 6.
“Kwa
kuwa mafunzo yanayotolewa katika kituo hiki ni ya muda mrefu na mfupi,
taratibu za kukisajili kwenye Baraza la taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE)
zilifanywa na kwa sasa kituo kimepata usajili wa kudumu wenye Na.
REG/SAT/003,” ameongea Mpesa.
Mpesa
ameongeza kuwa, wizara iliamua kuwekeza katika Kituo hicho kwa lengo la
kutoa mafunzo ya kuongeza thamani madini ya vito kwa wadau na
wajasiliamali wa madini hayo hapa nchini.
Ameongeza
kuwa, malengo mengine ni pamoja na kukuza na kuendeleza ujuzi na
ufahamu wa kutambua madini ya vito, kuongeza thamani kipato na ajira kwa
watanzania.
“
Hivi sasa kituo hicho kinatoa mafunzo ya muda mfupi ya ukataji na
unga’rishaji wa madini ya vito na kinaendesha shughuli za uchongaji wa
mawe ya miamba kwa kutengeneza wanyama, ndege, samaki na vitu
mbalimbali vya mapambo, amesema Mpesa.
Kituo
cha Jemolojia Tanzania (Tanzania Gemological Center -TGC) kilianzishwa
mwaka 2003 wakati serikali ikitekeleza mradi wa Maendeleo Sekta ya
Madini ( Mineral Sector Development Technical Assistance – MSD TA) ambao
ulitekelezwa kati yam waka 1994 na 2005 kwa mkpo kutoka benki ya Dunia.
Wakati huo lengo la kuanzissha kituo hicho lilikuwa ni kutekeleza Sera
ya Madini ya Mwaka 1997 kuhusu uongezaji thamani madini nchini kwa
kuanzia na kutoa mafunzo ya uchongaji wa vinyago vya miamba.
No comments:
Post a Comment