Benki
kuu ya Tanzania (BoT) inakanusha taarifa potofu zinazozosambazwa
kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii zikidai kuwa Benki Kuu
imechapisha noti zenye thamani ya shilingi trilioni 1.5 kwa ajili ya
matumizi ya serikali.
Benki
Kuu inauarifu Umma kuwa, taarifa hiyo sio sahihi na inalenga kuathiri
imani ya Wananchi na wadau wa kimataifa kuhusu uthabiti wa fedha ya
Tanzania.
Aidha,
Benki Kuu inawaasa Wananchi kuwa utoaji wa taarifa potofu kuhusu sekta
ya fedha unaweza kuleta athari kubwa kwa mwenendo wa uchumi.
Hivyo ni vyema Wananchi wajue yafuatayo kuhusu utoaji wa fedha kwa matumizi ya Serikali:
1.Mapato
ya serikali hayawiani moja kwa moja na matumizi yake mwezi-hadi-mwezi.
Kuna wakati mapato yanakuwa makubwa mfano miezi ya mwisho wa robo mwaka
na wakati mwingine yanakuwa madogo. Kwa sababu ya kupishana kwa mapato
na matumizi ya serikali, sheria imeruhusu serikali kuchukua mkopo wa
muda mfupi kutoka Benki Kuu ili kuziba pengo pale linapotokea na
kurejesha baadaye. Utaratibu huu unatumika duniani pote na hapa Tanzania
sheria inairuhusu Serikali kukopa kutoka Benki Kuu kwa vipindi vifupi
hadi ukomo wa asilimia 12.5 ya mapato ya ndani ya serikali ya mwaka
uliotangulia.
2.Ili
kupata picha halisi ya utekelezaji wa bajeti ya serikali na hali ya
deni la Taifa, ni vyema kuangalia mwenendo mzima katika kipindi cha
miezi kumi na mbili ya mwaka wa fedha husika, badala ya kuangalia mwezi
mmoja mmoja, ambapo kuna mabadiliko ya kimsimu. Mtazamo wa mwaka mzima
hutoa uhalisia wa mapato na matumizi, na ongezeko la deni lililohitajika
kuwezesha utekelezaji wa bajeti ya serikali katika kipindi hicho.
Taarifa ya kila mwezi ya uchumi ya Benki Kuu toleo la mwezi Julai
inaonesha kwamba mkopo wa muda mfupi (overdraft) wa Benki Kuu kwa
serikali uliongezeka kutoka shilingi bilioni 610.0 mwezi Mei 2018 hadi
shilingi bilioni 1,937.4 mwezi Juni 2018, sawa na ongezeko la shilingi
bilioni 1,327.4. Ongezeko hili halipaswi kuangaliwa kama tukio la mwezi
Juni 2018 pekee kwani taarifa hiyohiyo inaonesha kuwa kati ya mwezi Juni
2017 na mwezi Mei 2018 overdraft ya Benki Kuu ya Tanzania kwa serikali
ilipungua kwa shilingi bilioni 936.6, kutoka shilingi bilioni 1,546.6
hadi shilingi bilioni 610.0. Kupungua huku kulichangiwa na mapato ya
kawaida ya serikali pamoja na mikopo kutoka nje ya nchi.
3.Aidha,
Benki Kuu haijachapisha noti mpya katika kipindi hiki, hata hivyo noti
mpya, hazichapishwi kiholela ili kutoa pesa kwa serikali, bali
huchapishwa kulingana na taratibu za kisheria. Kwa kawaida utengenezaji
wa noti na sarafu huanza baada ya kukamilika kwa mchakato wa usanifu wa
michoro, aina ya karatasi itakayotumika, alama za utambulisho wa nchi
pamoja na alama za usalama. Na mara baada ya kukamilika kwa mchakato
huo, Benki Kuu huandaa kiasi gani kitakachoweza kutosheleza mahitaji ya
nchi kwa kipindi maalum kwa kuzingatia ukuaji wa pato la Taifa, Mfumuko
wa bei na pia kufidia fedha zilizochakaa ambazo hazipaswi kurudi katika
mzunguko na kiasi kilichobaki (buffer stock) ili kutosheleza kipindi
chote cha mchakato wa uchapishaji.
Benki
kuu inawaasa Wananchi kutotoa taarifa zisizo za kweli zenye lengo la
kuupotosha Umma na kusababisha hofu na kupoteza imani juu ya uthabiti wa
fedha ya Tanzania na badala yake wawe wanaomba kupewa taarifa kutoka
Taasisi husika.
BENKI KUU YA TANZANIA
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
11 Septemba, 2018
No comments:
Post a Comment