Mkuu
wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, akiongea jambo wakati akifungua rasmi
mafunzo ya siku mbili kuhusu masuala ya jotoardhi kwa washirki kutoka
nchi zilizo katika bonde la Ufa . Mafunzo hayo yanatangulia kabla ya
ufunguzi rasmi wa Kongamano la Tano la Kimataifa la Jotoardhi
litakalofunguliwa tarehe 29 Oktoba, 2014 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal.
Baadhi
ya washiriki wanaohudhuria mafunzo kuhusu masuala la jotoardhi,
wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela (hayupo pichani),
wakati akifungua rasmi mafunzo hayo.
Mkuu
wa Wilaya ya Arusha, John Mongela (katikati), akiongea jambo na Kamishna
Msaidizi anayeshughulia Nishati Jadidifu, Wizara ya Nishati na Madini,
Edward Ishengoma (kushoto), mara baada ya kufungua mafunzo kuhusu masuala
yanayohusu jotoardhi.
Baadhi
ya Washiriki wa mafunzo ya masuala ya jotoardhi, kutoka nchi zilizo
katika bonde la ufa na nyingine Duniani, wakiwa katika picha ya
pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela (wanne kulia).
Na Mwandishi wetu.
Imeelezwa kuwa, nguvu ya nishati mchanganyiko ikiwemo jotoardhi
ni kichocheo na kipimo cha maendeleo kwa nchi yoyote kutokana na umuhimu
wa nishati hiyo kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za uchumi na viwanda.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha John Mongela
wakati akifungua mafunzo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa
Mulongo, kuhusu masuala yanayohusu jotoardhi yaliyoanza leo katika
Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Mafunzo hayo yanashirikisha washiriki takriban 150 kutoka nchi
mbalimbali za Afrika zilizo katika bonde la ufa na nchi nyingine
duniani.
Aidha ameongeza kuwa, mafunzo hayo ni muafaka kwa Tanzania
kutokana na uzoefu ambao washiriki wataupata kutoka nchi nyingine ambazo
zimepiga hatua katika masuala ya jotoardhi kama Kenya na Ethiopia
ambazo zimechangia katika gridi ya Taifa ya nchi zao kiasi cha megawati
500 za nishati ya umeme unaotokana na jotoardhi.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia
nishati jadidifu, Wizara ya Nishati na Edward Ishengoma, ameeleza kuwa,
mafunzo hayo na uwepo wa kongamano hilo kwa Tanzania kuna manufaa
makubwa.
Ishengoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya
Kongamano la tano la Kimataifa la Jotoardhi alitaja manufaa hayo kama
kutangaza hazina kubwa ya jotoardhii iliyopo Tanzania, jambo ambalo
litasaidia kuvutia wawekezaji na taasisi zinazofanya utafiti wa masuala
ya jotoardhi.
Ameongeza kuwa, nishati ya jotoardhi ni nishati isiyokwisha
hivyo uwepo na matumizi yake yatasaidia katika ukuaji wa viwanda ikiwemo
kuchangia katika sekta za kilimo na manufaa yake ni makubwa
kimaendeleo.
“Jotoardhi ni chazo ambacho hakiishi. Uzalishaji wake hauna
mwisho na una manufaa makubwa. Tanzania tunataka kukiendeleza chanzo
hiki kama wenzetu Kenya na Ethiopia”amesisitiza Ishangoma.
Aidha, mafunzo hayo ni mwendelezo wa shughuli mbalimbali
zitakazofanyika katika kongamano la tano la Kimataifa la Jotoardhi
litakalofunguliwa rasmi tarehe 29 Oktoba, 2014, na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal.
Washiriki wa kongamano hilo pia watapata fursa ya kutembelea
katika maeneo yenye dalili za jotoardhi ikiwemo Ngorongoro na Manyara
lakini pia watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii
vilivyopo nchini.






No comments:
Post a Comment