Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala wa Baraza la Mitihani la Tanzania
(NECTA), Bw. Daniel Mafie (kushoto), akiwaeleza Waandishi wa Habari jana Jijini Dar
es salaam, kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na Baraza hilo ikiwemo matumizi
ya TEHAMA katika usajili wa watahimiwa na uchakataji wa matokeo ya
Mitihani ya Taifa. Kulia ni Afisa Habari wa NECTA John Nchimbi.
Mkuu
wa Idara ya Fedha na Utawala wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA),
Bw. Daniel Mafie (katikati), akiwaeleza Waandishi wa Habari jana Jijini Dar s salaam,
kuhusu utaratibu wa kutoa nakala za vyeti kwa watahimiwa waliopoteza
vyeti vyao, ambapo utaratibu huo unahusisha uchunguzi wa uhalali wa
mwombaji. Kulia ni Afisa Habari wa NECTA, John Nchimbi na kushoto ni
Msaidizi wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Bi. Glee
Magemba.
Na Mwandishi wetu.
Baraza la Mitihani la Tanzania
(NECTA), limedhibiti na kuondoa kabisa tatizo la wizi wa Mitihani ya
Taifa na udanganyifu wakati wa Mitihani katika ngazi mbalimbali za elimu
nchini.
Mafanikio hayo yametokana na
ushirikiano uliopo kati ya NECTA na kamati za uendeshaji mitihani katika
ngazi za mikoa na wilaya ili kutatua tatizo la wizi wa mitihani ya
taifa na udanganyifu wakati wa mitihani uliokuwa ukifanywa kinyume na
taratibu za baraza la mitihani.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara
ya Fedha na Utawala wa Baraza hilo, Bw. Daniel Mafie, wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari Jjijini Dar es salaam, uliolenga kueleza
mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa.
Akifafanunua Mafie amesema kuwa,
katika mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2013 watahimiwa
waliofutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu walikuwa 13 tu
ikilinganishwa na watahiniwa 9,736 waliobainika kufanya udanganyifu
mwaka 2011.
Aidha Mafie aliongeza kuwa,
katika Mtihani wa Kidato cha nne mwaka 2013 watahimiwa waliofutiwa
matokeo kwa kufanya udanganyifu walikuwa 272 ikilinganishwa na
watahimiwa 789 mwaka 2012 na 3,303 mwaka 2011.
Akieleza zaidi kuhusu mafanikio
yaliyofikiwa Mafie alisema Baraza hilo limeweza kusanifu mifumo ya
Kompyuta yenye uwezo wa kupanga shule katika makundi ya ubora wa ufaulu
katika matokeo ya mitihani ya Taifa.
Katika kukabiliana na tatizo la
watu wanaotumia vyeti vya watu wengine au kughushi vyeti wakati wa
kuomba ajira au nafasi za masomo katika shule mbalimbali ambapo kuanzia
mwaka 2008/2009 Baraza hilo lilianzisha utaratibu wa kuweka picha za
watahimiwa katika vyeti vyao.
Katika utaratibu huo vyeti hivyo
viliwekewa alama za kiusalam hali ambayo imesaidia Baraza hilo kuwa na
uwezo wa kubaini kwa haraka na kuwachukulia hatua wale wanaoghushi vyeti
au kutumia vyeti vya watu wengine.
Baraza la Mitihani la Tanzania
ni Taasisi ya Umma iliyochini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
iliyoanzishwa kwa sheria ya Bunge Namba 21 ya mwaka 1973, na marekebisho
yake ya mwaka 1998 na 2002 kwa ajili ya kuendesha mitihani ya Taifa kwa
lengo la kuweka misingi ya sera ya mitihani, kuendesha mitihani na
kutunuku stashahada mbalimbali na vyeti kwa watahiniwa wanaofuzu na
kufaulu mitihani iliyo chini yake kisheria.




No comments:
Post a Comment